KIKWETE AWANOA MAWAZIRI CHUO KIKUU CHA HARVARD
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, yuko jijini Boston, Marekani, ambapo anashiriki katika kutoa mafunzo maalum kwa viongozi wa ngazi za juu kutoka mataifa mbalimbali yanayoendelea kupitia Mpango wa Uongozi wa Ngazi ya Mawaziri wa Harvard (Harvard Ministerial Leadership Program).
Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Chuo Kikuu cha Harvard, yanalenga kuimarisha uwezo wa viongozi katika kusimamia sera na kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika mataifa yao.
Katika programu hiyo, Dkt. Kikwete anashiriki kama mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu wenye uzoefu wa kipekee, akiwa na sifa ya kipekee ya kuwa aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha kati ya mwaka 1994 na 1995 kabla ya kushika madaraka ya juu ya nchi.
Uzoefu huo unamfanya kuwa mbobezi wa kiwango cha juu anayefundisha kutokana na uelewa wa moja kwa moja wa changamoto zinazowakabili Mawaziri wa Fedha na wa Mipango katika usimamizi wa rasilimali na kukuza uchumi.
Mbali na Rais Mstaafu Kikwete, mafunzo hayo yanashirikisha pia wakuu wa taasisi za kimataifa, viongozi kutoka mashirika binafsi, na wabobezi wa masuala ya sera na uchumi duniani. Wadau hao wameungana ili kubadilishana uzoefu wa kivitendo na nadharia za kisasa zinazoweza kusaidia kutatua changamoto za kiuchumi zinazoyakabili mataifa yanayoendelea, hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi duniani.
Tanzania imewakilishwa vyema katika mafunzo hayo na viongozi watatu waandamizi ambao ni Waziri wa Fedha, Mhe. Khamis Mussa Omar, pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo. Aidha, upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umewakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Juma Malik Akil, ambapo kwa pamoja wanatarajiwa kunufaika na mbinu mpya za usimamizi wa mipango ya kitaifa.
Ushiriki wa viongozi hawa unalenga kuimarisha uwezo wa serikali katika kuratibu sera za uwekezaji na mipango ya maendeleo ya muda mrefu. Uwepo wa Dkt. Kikwete kama mkufunzi unatoa fursa adhimu kwa viongozi hao wa Tanzania na wenzao kutoka nchi nyingine kujifunza kutoka kwa kiongozi aliyepitia ngazi zote za uamuzi, kuanzia usimamizi wa hazina ya nchi hadi kufikia uongozi wa juu wa kitaifa.
Post a Comment