KIKWETE AKUTANA NA SIMBU, AMPONGEZA KWA USHINDI MARATHONI YA BOSTON



Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amekutana na kumpongeza mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu, kufuatia ushindi wake mkubwa wa kushika nafasi ya pili katika Mashindano ya Riadha ya Boston (Boston Marathon) mwaka 2026.

Ushindi huo wa Simbu ni heshima kubwa kwa taifa la Tanzania, ukiweka jina la nchi katika ramani ya juu ya michezo duniani kwenye moja ya mbio kongwe na zenye ushindani mkubwa zaidi duniani. Dkt. Kikwete amemuelezea Simbu kama mfano wa kuigwa kwa vijana wa Kitanzania kutokana na juhudi na uzalendo aliounyesha.

Dkt. Kikwete yuko jijini Boston kwa majukumu mengine muhimu ya kimataifa. Rais huyo mstaafu anashiriki kama mkufunzi katika Mpango wa Uongozi wa Ngazi ya Mawaziri wa Harvard (Harvard Ministerial Leadership Program), unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Harvard.



Katika mpango huo, Dkt. Kikwete anatoa mafunzo kwa Mawaziri wa Fedha na Mipango kutoka nchi mbalimbali zinazoendelea, akitumia uzoefu wake adhimu wa kuwa Waziri wa Fedha wa zamani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. Kikwete ni miongoni mwa viongozi wakuu wastaafu wachache duniani waliochaguliwa kutoa muongozo wa kistratejia kwa viongozi hao huko Harvard.

Hivyo, jijini Boston imekuwa ni wiki ya fahari kwa Tanzania; mwanariadha wetu akitwaa fedha barabarani na kiongozi wetu mstaafu akishiriki kutoa maarifa kwenye jukwaa la juu la kitaaluma duniani.

No comments