WAFCON 2026 SASA KUFANYIKA MOROCCO JULAI HADI AGOSTI




Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) sasa yanatarajiwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Julai 25 hadi Agosti 16, mwaka huu. 

Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) hapo awali lilipanga michuano hiyo kuanza Machi 17 hadi Aprili 3, 2026, lakini tarehe hizo zilisogezwa mbele kufuatia maombi ya wenyeji na majadiliano ya kina na wadau mbalimbali.

Katika taarifa iliyotolewa na CAF hivi karibuni, ilielezwa kuwa uamuzi wa kupanga upya tarehe hizo umefikiwa baada ya mashauriano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) pamoja na washirika wengine. 

Lengo kuu la mabadiliko hayo ni kuhakikisha mafanikio ya mashindano haya muhimu kwa kuzingatia hali fulani zisizotarajiwa, huku wahusika wote wakionyesha imani kubwa kuwa maandalizi yanayofanyika yataleta matokeo chanya.

Mabadiliko haya ya ratiba yanaigusa moja kwa moja timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, inayojiandaa kushiriki fainali hizo kwa mara ya tatu. 

Katika historia yake, Twiga Stars ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kuishia hatua ya makundi bila pointi, huku katika michuano ya WAFCON 2024 iliyofanyika mwaka jana nchini Morocco, walimaliza mkiani mwa Kundi C wakiambulia sare moja pekee.

Kwa sasa, Twiga Stars inaendelea na kambi ya maandalizi ambapo baada ya kutokea nchini Misri, imehamishia makali yake Dubai kushiriki michuano maalumu ya kirafiki iliyoandaliwa na FIFA.

 Katika michuano hiyo inayoshirikisha mataifa ya Urusi, Ghana, na Hong Kong, Twiga Stars tayari imecheza mchezo mmoja na kupoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Urusi, huku timu ya Ghana ikionekana kung'ara zaidi baada ya kushinda michezo yake dhidi ya Hong Kong na Urusi.

No comments