TRC YATOA MSAADA WA CHAKULA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO KILOMBERO

 


Wananchi wa kata za Kibaoni, Michenga, Lumemo na Lipangalala zilizopo katika Halmashauri ya mji wa Ifakara, Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro, wamepata nafuu ya kimaisha baada ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufika eneo hilo kutoa mkono wa faraja kufuatia majanga ya asili yaliyowasibu. 

Shirika hilo limekabidhi msaada wa tani moja ya unga wa mahindi kwa lengo la kupunguza makali ya maumivu na changamoto za kijamii zinazowakabili wananchi hao baada ya kukumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zisizo za kawaida zilizonyesha mfululizo usiku wa Machi 24 na 25, 2026.

Msaada huo wa kiutu umepokelewa rasmi na Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Mheshimiwa Abubakari Asenga, katika hafla fupi iliyofanyika kijijini Kibaoni na kushuhudiwa na mamia ya wananchi waliopoteza baadhi ya mali na akiba zao za chakula kutokana na maji kuingia kwenye makazini. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa kata hizo akiwemo Januari Haule wa Lumemo na Margreth James wa Michenga, wamelishukuru shirika hilo kwa kuwakumbuka katika kipindi hiki kigumu, wakibainisha kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuziba pengo la chakula wakati wakisubiri hali ya hewa kutengamaa ili kurejea katika shughuli zao za kila siku za kujiingizia kipato.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TRC, Fredy Mwanjala, amebainisha kuwa shirika hilo linatambua fika kuwa msaada uliotolewa hauwezi kuondoa maumivu na hasara zote walizopata wananchi, lakini ni ishara ya dhati ya mshikamano kati ya taasisi hiyo na jamii ya wana-Kilombero. 

Mwanjala amesisitiza kuwa TRC kama mdau mkubwa wa maendeleo nchini, inaguswa na majanga yanayowafika wananchi na imejidhibiti kusimama bega kwa bega na waathirika katika nyakati zote za shida na raha ili kuhakikisha huduma na ustawi wa jamii unarejea katika hali yake ya kawaida mapema iwezekanavyo.

Athari za mvua hizo za Machi 24 na 25 hazikuishia kwenye makazi ya watu pekee, bali zimesababisha changamoto kubwa ya usafiri baada ya kukatika kwa barabara kuu inayounganisha Ifakara na Mlimba katika maeneo ya kimkakati ya Chita, Mbingu na Chage. 

Hali hiyo imesababisha adha ya mawasiliano kwa wasafiri na wasafirishaji wa bidhaa, jambo linalofanya jitihada za taasisi kama TRC kuonekana kuwa na tija kubwa kwa sasa. 

Mheshimiwa Asenga amewahakikishia wananchi kuwa serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea ili kuchukua hatua stahiki za kurejesha miundombinu hiyo muhimu huku akiwashukuru TRC kwa moyo wao wa uungwana uliogusa mioyo ya wananchi wa Kilombero.

No comments