RAIS SAMIA ALILIA SABA WA AFYA



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, kufuatia vifo vya watumishi saba wa afya vilivyotokea katika ajali ya boti kwenye Ziwa Tanganyika.

Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Samia ameeleza kuguswa na vifo hivyo vilivyotokea wakati watumishi hao walipokuwa wakienda kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma za afya kuelekea Kijiji cha Kagunga, mpakani mwa Tanzania na Burundi.

“Ninatoa pole za dhati kwa familia, ndugu na jamaa wa wote waliopoteza maisha katika ajali hizi,” amesema Rais Dkt. Samia kupitia taarifa hiyo, huku akiwaombea majeruhi 14 wanaoendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni wapone haraka.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 2:00 asubuhi katika eneo la Kijiji cha Kalalangabo, Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya boti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kupigwa na upepo mkali na dhoruba na kusababisha kupinduka.

Ripoti kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa watumishi hao saba waliofariki ni pamoja na wanaume wanne na wanawake watatu. Aidha, juhudi za uokoaji zinaendelea kuwatafuta watu wawili ambao bado hawajapatikana tangu kutokea kwa ajali hiyo.

Mbali na ajali ya boti, Rais Samia pia ametoa pole kwa kifo cha mvuvi mmoja kati ya watatu waliokuwa kwenye mtumbwi ambao ulipigwa na radi ziwani huko mkoani Kigoma, tukio lililosababisha wavuvi wengine wawili kujeruhiwa.

Kufuatia mfululizo wa matukio hayo ya majanga ziwani, Rais ametoa rai kwa wananchi na wasafiri wanaotumia vyombo vya majini, hususan wavuvi, kuongeza tahadhari dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo upepo mkali na radi.

Mapema  Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, aliongoza dakika moja ya ukimya kuwaombea watumishi hao, akibainisha kuwa wizara imepoteza mashujaa waliojitolea kuhudumia jamii katika mazingira magumu ya mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewahakikishia wananchi kuwa serikali ipo karibu na familia za wahanga na itatoa msaada wote unaohitajika katika kipindi hiki cha majonzi.


No comments