MAKONDA APIGA MKWARA MZITO: Atikisa Mashirikisho ya Michezo, Ataka Matokeo au Wang’oke




WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ametoa onyo kali kwa viongozi wa mashirikisho ya michezo nchini, akitishia kuwaondoa madarakani wale wote walioshindwa kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wanachama wao wakati wa kampeni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Makonda amesema ofisi yake itaanza kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo kwa ukaribu zaidi. Amesema endapo itabainika kiongozi ameshindwa kufikia hata asilimia 20 ya yale aliyoahidi, wizara itashirikiana na wanachama kuleta mabadiliko ya uongozi mara moja.

“Nyinyi mlipata nafasi hizi kwa kupigiwa kura na wanachama wenu. Ni lazima mjiulize mmetimiza kwa kiwango gani ahadi mlizotoa. Serikali haitaridhika kuona viongozi wanaendelea kushikilia madaraka bila kuonyesha matokeo yanayogusa maendeleo ya michezo,” alisisitiza Makonda.

Katika hatua nyingine, Waziri Makonda amewatolea uvivu viongozi wanaotumia mbinu za kubadilisha katiba za mashirikisho ili kulinda maslahi yao binafsi na kusalia madarakani kwa muda mrefu. Amesema ana taarifa za baadhi ya viongozi waliokaa madarakani kwa zaidi ya miaka 15 kwa kufanya marekebisho ya katiba yanayowabeba wao badala ya taasisi.



“Naambiwa kuna watu wamekaa kwenye nafasi miaka zaidi ya 15 kwa kubadilisha katiba kila mara ili iwafae wao kubaki madarakani. Katiba lazima ziwe wazi na zenye kulinda maslahi ya wanachama na si viongozi wachache,” alisema.

Kufuatia hali hiyo, Makonda ametoa maagizo ya papo kwa papo akitaka Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kukabidhiwa ofisi ndani ya saa 24. Aidha, amemtaka Msajili wa Vyama vya Michezo kuhakikisha Katiba ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) inatoka na kukabidhiwa kwa wahusika ifikapo Jumatatu ijayo.

Waziri huyo alihitimisha kwa kuwataka viongozi hao kuimarisha uwazi na kushughulikia migogoro ya ndani ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya michezo nchini, akisisitiza kuwa jukumu lake kuu ni kuhakikisha sekta hiyo inaleta matokeo chanya kwa taifa.

No comments