DARASA LA DURBAN: KIOO CHA MAGEUZI YA BANDARI YA DAR ES SALAAM NA USHINDI WA SEKTA BINAFSI
Ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, katika Bandari ya Durban nchini Afrika Kusini imetoa jibu la kijasusi na kiuchumi kwa wale waliokuwa na shaka juu ya uamuzi wa Tanzania kukaribisha uwekezaji wa sekta binafsi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Durban, ambayo ni miongoni mwa bandari kubwa na zenye ufanisi zaidi barani Afrika ikihudumia makasha milioni 2.6 kwa mwaka, imeonyesha kuwa hata mataifa yaliyopiga hatua kubwa kiviwanda yanatambua kuwa serikali pekee haiwezi kubeba mzigo wa uendeshaji wa kisasa bila ushirika wa kimkakati na makampuni yenye uzoefu wa kidunia.
Ushahidi wa wazi wa mwelekeo huu mpya wa kidunia umejidhihirisha Januari 2026, ambapo Bandari ya Durban imeingia mkataba wa miaka 25 na kampuni ya kimataifa ya ICTSI kwa ajili ya kuendesha sehemu ya Pier 2.
Hatua hii ya Afrika Kusini, taifa lenye uchumi mkubwa zaidi kusini mwa jangwa la Sahara, inashabihiana moja kwa moja na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Tanzania kukodisha sehemu ya bandari yake kwa kampuni kama DP World na Adani Ports kupitia TEAGTL/TICTS. Hii ni dhihirisho tosha kuwa Tanzania haikukosea, bali ilitangulia kuona mbali na kujipanga kabla ya ushindani wa kikanda haujawa mkali zaidi.
Alichokiona Kihenzile Durban ni namna uwekezaji wa sekta binafsi unavyoongeza kasi ya utendaji kwa zaidi ya mara mbili, jambo ambalo ndilo linafanyika sasa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kupitia ushirikiano huu wa sekta ya umma na binafsi (PPP), Bandari ya Dar es Salaam inabadilika kutoka kuwa kituo cha kupokelea mizigo tu na kuwa lango la kisasa lenye uwezo wa kushindana na bandari nyingine kubwa duniani. Uzoefu wa Durban unathibitisha kuwa kuleta teknolojia mpya, mitaji, na mifumo ya kisasa ya kidijitali kutoka kwa washirika wa nje ni hitaji la lazima ili kuongeza ufanisi wa gati na kuhudumia nchi za maziwa makuu kwa haraka zaidi.
Zaidi ya uendeshaji wa bandari, ziara hiyo imesisitiza umuhimu wa kuunganisha bandari na miundombinu imara ya reli kama Standard Gauge Railway (SGR), MGR, na TAZARA.
Serikali ya Tanzania tayari imeshaanza kutekeleza mnyororo huu wa thamani, ambapo umeme na kasi ya SGR vitaungana na ufanisi wa DP World bandarini ili kuhakikisha mzigo unatoka melini hadi nchi jirani ndani ya muda mfupi. Huu ni mkakati wa kijasusi wa kiuchumi unaoifanya Tanzania kuwa "hub" ya usafirishaji, ikitumia jiografia yake ya kipekee kuvutia biashara nyingi zaidi kutoka mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.
Alichokiona Naibu Waziri Kihenzile nchini Afrika Kusini ni uthibitisho kuwa dunia ya sasa haitaji kelele bali inahitaji matokeo, na matokeo hayo yanapatikana kwa kufungua milango kwa washirika makini. Tanzania imeshuka dimbani ikiwa na wachezaji wa daraja la kwanza kama DP World, ikifuata nyayo za Durban ambazo sasa nazo zimeamua kufuata njia hiyohiyo ya kukodisha makampuni ya nje.
Huu ni ushindi kwa sera ya diplomasia ya kiuchumi ya serikali, inayolenga kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa injini kuu ya Pato la Taifa na kitovu cha ajira na utajiri kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment