Rais Dkt. Samia Afungua Soko la Kariakoo, Aagiza Uwazi Upangaji wa Vizimba




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefungua rasmi Soko Kuu Jipya la Kariakoo jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua kubwa ya kurejesha mhimili huo wa biashara baada ya soko la awali kuteketea kwa moto mwezi Julai mwaka 2021. 

Katika ufunguzi huo uliofanyika  tarehe 8 Februari 2026, Rais amesisitiza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali kuimarisha mazingira ya biashara, kulinda mitaji ya wananchi, na kuongeza tija katika uchumi wa kitaifa na kikanda.

Akizungumza na viongozi pamoja na wananchi waliojitokeza, Rais Samia ametoa maelekezo mazito kwa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kuhakikisha mchakato wa kupanga maeneo ya biashara unafanyika kwa haki, usawa, na uwazi wa hali ya juu. 




Rais amepiga marufuku tabia ya viongozi kuhodhi vizimba na kuvikodisha kwa watu wengine, akielekeza kuwa Shirika la Masoko ya Kariakoo ndilo linapaswa kukodisha maeneo hayo moja kwa moja kwa wafanyabiashara. 

Amesititiza kuwa ni lazima kuwapa kipaumbele wafanyabiashara waliokuwepo awali ili kuzuia mianya ya upendeleo na kulinda maslahi ya wanyonge.

Aidha, Rais amehimiza uongozi wa soko kuimarisha mifumo ya kidijitali katika kukusanya mapato na kutoa huduma, huku akizitaka taasisi husika kusimamia ubora wa bidhaa kwa viwango vya kimataifa. 





Rais ameelezea kufurahishwa kwake na miundombinu rafiki kwa wanawake, ikiwemo vyumba vya kunyonyeshea, lakini amekwenda mbali zaidi kwa kutoa rai kwa menejimenti kutenga eneo maalum la kulelea watoto kwa ajili ya akina mama wafanyabiashara sokoni hapo.

Soko la Kariakoo linaelezwa kuwa ni injini muhimu ya uchumi nchini, likichangia wastani wa shilingi bilioni 13 kila mwezi kama mapato ya ndani ya moja kwa moja, na zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa njia zisizo za moja kwa moja kupitia mifumo mbalimbali ya kodi. Rais amehitimisha kwa kutoa wito kwa watumiaji wa soko hilo kulilinda na kulitunza kama uwekezaji wa kimkakati utakaosaidia kukuza ajira na uzalishaji nchini kote.

No comments