Mashabiki na wachambuzi waizungumza dabi ya Kariakoo


Msisimko wa dabi ya kihistoria ya Kariakoo iliyopigwa Machi 1, 2026 katika uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, umeacha mwangwi mpana miongoni mwa wachambuzi na wadau wa soka nchini baada ya miamba hiyo ya soka kumalizika kwa sare ya 0-0. 

Mchambuzi nguli wa soka, Ibrahim Masoud maarufu kama Maestro, ametoa mtazamo wake akisema kuwa Yanga walizidiwa kete kwa kiasi kikubwa katika eneo la kiungo na umiliki wa mpira, huku akisisitiza kuwa licha ya uzoefu wa kikosi cha Yanga, walishindwa kuhimili kasi na presha kubwa iliyowekwa na Simba katika kipindi chote cha mchezo.

Hali hiyo ya ushindani ilionekana mapema tangu kuanza kwa mchezo, ambapo dakika ya 40 Yanga walilazimika kufanya mabadiliko ya mapema baada ya nahodha wao, Dickson Job, kupata majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na Bakari Nondo Mwamnyeto. 

Mchambuzi Yahya Mohammed "Mkazuzu" amekiri kuwa dabi hiyo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu uliopitiliza matarajio ya wengi, huku akisifu namna timu zote zilivyojipanga kimbinu kuzuia wapinzani wao wasipate mwanya wa kufunga mabao.



Kwa upande wa viongozi na wadau wa siasa, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, Ussi Salum Pondeza, ameeleza kuridhishwa kwake na kiwango kilichooneshwa na klabu ya Simba akitaja nidhamu na ari ya kupambana kama chachu ya matokeo hayo ya sare. 

Hata hivyo, shabiki maarufu wa Yanga, Mark Yanga, amekiri kuwa mchezo huo ulikuwa na milima na mabonde huku akiwaonya mashabiki wenzake kutoidharau Simba kwa kuwa walionesha uwezo mkubwa wa kupambana ndani ya uwanja.

Licha ya presha hiyo, upande wa mashabiki wa Yanga kupitia kwa Fumau Mshairi, wamepokea sare hiyo kama sehemu ya mafanikio ya klabu yao kuelekea ubingwa. Fumau amesisitiza kuwa malengo makuu ya Yanga ni kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC na kulinda rekodi ya kutokufungwa, jambo ambalo limefanikiwa kwa kupata alama hiyo moja muhimu iliyowafanya waendelee kukaa kileleni mwa msimamo wakiwaacha Simba kwa tofauti ya alama tano.

Jambo lingine lililoibua gumzo la kipekee katika dabi hiyo ni hali ya usalama na amani iliyojitokeza uwanjani, ambapo mchambuzi Shaffih Dauda ameeleza kushangazwa na kufurahishwa na kitendo cha mashabiki wa timu hizo mbili kukaa pamoja kwenye majukwaa. Dauda amesifu ukomavu na mshikamano uliooneshwa na mashabiki hao visiwani Zanzibar, akieleza kuwa kitendo hicho ni mfano wa kuigwa katika soka la Tanzania ambalo mara nyingi huambatana na uhasama mkubwa majukwaani.

Mwisho wa mchezo huo umewacha Simba wakiwa na kazi ya ziada ya kupunguza pengo la alama tano dhidi ya wapinzani wao, huku Yanga wakiondoka New Amaan Complex kwa kicheko cha kuendelea kutawala msimamo wa ligi. 

Wadau wengi wamehitimisha kuwa dabi hii imeweka historia mpya kwa kuchezwa Zanzibar na kuonesha kuwa soka la Tanzania limeendelea kukua kwa kasi kifikra, kiufundi na hata katika hali ya kiungwana miongoni mwa washabiki.

No comments