KIKWETE:MAONO YA RAIS SAMIA YAMELETA MAPINDUZI MAKUBWA KINGA YA JAMII

 


Tanzania imeandika rekodi mpya ya kihistoria katika sekta ya Kinga ya Jamii! Hatua hii imekuja baada ya nchi yetu kutajwa rasmi kuwa miongoni mwa nchi 17 duniani zenye mifumo bora zaidi ya hifadhi ya jamii. 

Mafanikio haya si ya bahati mbaya, bali ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayolenga kuinua ustawi wa kila Mtanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Nchi Ofisi ya Rais,Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete , wakati akihitimisha mkutano wa siku mbili wa wadau wa sekta ya Kinga ya Jamii jijini Arusha, Februari 10, 2026.

Waziri Kikwete ametaka kuwepo kwa utekelezaji wa kina wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kuhusu kinga ya jamii kwani tayari maono yake Rais Samia yamesababisha mafanikio makubwa .

Amewataka watekelezaji wa sera hiyo kujipanga vyema na kuweka nguvu katika kutekeleza dira na maono yaliyotolewa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. 

Aidha ametoa wito kwa watendaji wote kuyaishi maelekezo ya Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa kuhitimisha Bunge la kumi na mbili tarehe 27 Juni 2025 pamoja na kuzingatia ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na dira ya maendeleo.Amesema utekelezaji wa miongozo hiyo utasaidia kupata matokeo chanya katika kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii nchini. 

Mh Kikwete alisema kwambaTanzania inatekeleza misingi yote tisa ya hifadhi ya jamii ikiwemo fao la familia ambalo huko nyuma lilikuwa halijawekwa sawa lakini sasa linatekelezwa kupitia huduma za kijamii.

Alisema kwamba fao hilo la familia linajumuisha utoaji wa elimu bure, matibabu kwa wazee, matibabu kwa watoto pamoja na akina mama ambapo yote haya ni sehemu ya mchango wa Serikali kwa wananchi wake. 

Alisema ndoto ya Watanzania kuwa ndani ya mfumo wa hifadhi ya jamii sasa inakwenda kukamilika huku akipongeza taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali kwa kazi nzuri ya kuandaa nyaraka na miongozo muhimu kuhusu kinga ya jamii.



Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga  akimkaribisha waziri Kikwete alisema Mkutano huo wa siku mbili ulitoa fursa ya kipekee kwa wadau kujadili kwa kina kubadilishana uzoefu na maarifa yenye lengo la kuboresha sekta hiyo kwa ajili ya maendeleo ya taifa. 

Aidha alisema kwamba katika mkutano huo washiriki walijengeana uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa Kinga ya Jamii kwa maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa na kuangalia namna ya kuimarisha ushirikiano na uratibu kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo katika kuimarisha mifumo  ya kinga.

Katika kipindi cha siku mbili, washiriki wamepata fursa ya kupokea na kujadili mada mbalimbali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na taasisi za PSSSF, NSSF, WCF, NHIF na TASAF. Vilevile, tulipata mafunzo muhimu kuhusu uzingatiwaji wa mienendo ya maisha, hususan mapambano dhidi ya msongo wa mawazo na afya ya akili maeneo ya kazi.

Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu,ambaye alibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya kinga ya jamii nchini, ambapo thamani ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii imeongezeka maradufu kutoka shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi trilioni 24.20 mwezi Desemba 2025. 

Aidha alisema mafanikio hayo yameenda sambamba na uimarishaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao katika awamu ya pili pekee umeweza kunufaisha zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye takribani watu milioni 5.5 kwa ruzuku ya zaidi ya shilingi trilioni 1.55.

No comments