OFISI YA WAZIRI MKUU YAAHIDI KUFANYIA KAZI MAAZIMIO YA WADAU WA KINGA YA JAMII ARUSHA
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) imeahidi kufanyia kazi kwa weledi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii kwa maslahi mapana ya Taifa.
Ahadi hiyo imetolewa leo, Februari 10, 2026, jijini Arusha wakati wa kuhitimisha mkutano wa siku mbili uliowakutanisha wadau takribani elfu moja (1,000) kutoka nyanja mbalimbali nchini.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili ustawi wa sekta hiyo, sambamba na uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023 na Hifadhi ya Skimu kwa Waliojiajiri.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufunga mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Mary Maganga amesema maelekezo , maswali na maoni yaliyotolewa na wadau yatakuwa mwongozo mkuu katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo ili kuleta mapinduzi katika sekta ya hifadhi ya jamii.
Kufuatia majadiliano ya kina yaliyoanza tangu Februari 9, 2026, mkutano huo umeibua hoja nne za kimkakati ambazo wadau wamependekeza zipewe msukumo wa kiutendaji:
Ujumuishi wa Sekta Isiyo Rasmi: Wadau wameushauri Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuangalia uwezekano wa kuwajumuisha wananchi waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi ili nao wanufaike na mafao kama walivyo wafanyakazi wa sekta rasmi.
Mabadiliko ya Mitalaa ya Elimu: Kupendekeza masuala ya Kinga ya Jamii yaingizwe katika mitalaa ya elimu kuanzia ngazi ya Vyuo Vikuu ili kujenga utamaduni wa hifadhi ya jamii kwa vijana kabla ya kuingia kwenye soko la ajira.
Usimamizi wa Sheria: Waajiri wamekumbushwa wajibu wao wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kulinda haki za wafanyakazi na kuepuka migogoro isiyo ya lazima mahali pa kazi.
Elimu kwa Umma: Kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu endelevu kuhusu sheria, kanuni na miongozo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuondoa upotoshaji na sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Mkutano huo umetajwa kuwa kielelezo cha ushirikiano kati ya serikali na wadau katika kuimarisha ustawi wa watanzania. Ofisi ya Waziri Mkuu imewashukuru washiriki wote kwa utayari wao na imemshukuru Mgeni Rasmi kwa kutenga muda wake kusikiliza maazimio hayo na kutoa dira ya utekelezaji.

Post a Comment