TANZANIA HAIENDESHWI KWA ‘RIMOTI’, DKT. MWIGULU AFUNGUKA KUHUSU MARIDHIANO
Waziri wa Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa msimamo mkali dhidi ya wanaharakati wanaoishi nje ya nchi wanaopinga azma ya Serikali ya kuwa na maridhiano ya kitaifa, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi huru na haitayumba wala kuendeshwa kwa "rimoti" kutoka nje.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa maji katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Dkt. Mwigulu amewashutumu wanaharakati hao kwa kukosa mwelekeo na kusema kuwa vitendo vyao vinapingana na misingi na utamaduni wa Watanzania wa kupendana na kusikilizana.
Msimamo kuhusu Maridhiano
Dkt. Mwigulu amehoji uhalali wa watu wanaoishi nje ya nchi, ambao hawaguswi na hali ya usalama au amani ya ndani, kupinga mchakato wa maridhiano unaolenga kuunganisha Taifa.
"Nilimsikiliza mwanaharakati mmoja anasema hatutaki maridhiano; wewe hata Tanzania haupo, hauishi hapa wala ndugu zako hawapo hapa, unasema hutaki maridhiano kwani tunaridhiana na wewe kuhusu nini?" alihoji Dkt. Mwigulu.
Aliongeza kuwa tabia ya baadhi ya wanaharakati hao kutafuta sifa kwa kutukana viongozi na hata kushangilia misiba ni kinyume na uadilifu na utu wa Kitanzania.
Uchumi wa Ndani na Miradi ya Bilioni 46
Kuhusu hali ya uchumi, Dkt. Mwigulu amewahakikishia wananchi kuwa Tanzania ni nchi tajiri yenye uwezo wa kutumia rasilimali zake na fedha za ndani kukamilisha miradi mikubwa.
Mfano wa utajiri huo ni mradi wa maji wa Shilingi Bilioni 46.2 ambao unakwenda kunufaisha zaidi ya wakazi 450,000 wa Jiji la Mwanza na wilaya jirani za Magu na Misungwi.
Maeneo yatakayopata neema ya maji safi na salama ni pamoja na Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyahingi, Luchelele, Sahwa, Kishiri, Igoma, Kisesa, Bujora, Kanyama, Fela, na Usagara. Waziri huyo amewataka watendaji kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kuleta manufaa ya haraka kwa mwananchi.
Reli ya SGR na Maendeleo ya Elimu
Dkt. Mwigulu ametoa habari njema kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), akisema kuwa fedha za kuifikisha reli hiyo mkoani Mwanza zipo tayari na Serikali inasubiri tu mkandarasi akamilishe kazi ili alipwe.
"Siku si nyingi zijazo, tutakunywa chai Mwanza, chakula cha mchana tutakula Dodoma, na chakula cha jioni tutakula Dar es Salaam," alisema Dkt. Mwigulu, akionyesha jinsi miundombinu hiyo itakavyorahisisha maisha na kuchochea biashara.
Pamoja na hayo, Waziri huyo amewahimiza wazazi na walezi wa Kanda ya Ziwa kuhakikisha watoto wote walioandikishwa shule wanahudhuria masomo bila kukosa, kwani elimu ndiyo msingi wa kutengeneza viongozi bora wa baadaye watakaolinda na kuendeleza tunu za Taifa.
Post a Comment