SERIKALI YATANGAZA KIAMA KWA WANAOKWAMISHA MAGARI YA DHARURA NA WANAOTUMIA VING’ORA KINYUME CHA SHERIA
Serikali imetangaza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukwamisha chombo cha dharura barabarani ikiwa ni sehemu ya mkakati mpya wa kurejesha nidhamu na usalama wa raia.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Patrobas Katambi wakati wa ziara yake katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini Dodoma ambapo alisisitiza kuwa madereva wengi wamekuwa wakipuuza ving'ora vya magari ya dharura kama vile zimamoto na magari ya wagonjwa jambo ambalo ni kosa la kisheria.
Waziri Katambi ameeleza kuwa serikali iko katika hatua za mwisho za kuendesha kampeni maalum ya kudhibiti utitiri wa ving'ora vinavyowekwa kinyume cha sheria kwenye magari ya watu binafsi pamoja na matumizi ya namba za magari zisizotambuliwa na kanuni za usalama barabarani.
Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Naibu Waziri Ayoub Mohamed Mahmoud kiongozi huyo amewataka wananchi kuelewa kuwa kuchelewesha chombo cha dharura ni kuhatarisha maisha ya watu na mali zao kwani sekunde chache zinaweza kuleta tofauti kubwa katika uokoaji.
Aidha amefafanua kuwa lawama zinazoelekezwa kwa Jeshi la Zimamoto kuhusu kuchelewa kufika kwenye matukio mara nyingi zinachangiwa na changamoto za miundombinu ikiwemo ujenzi holela unaoziba njia pamoja na kutozingatiwa kwa kanuni za ujenzi zinazopaswa kuwezesha upatikanaji wa huduma za dharura.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mahmoud ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa jeshi hilo huku akipongeza kazi kubwa ya uokozi inayofanywa na askari nchi nzima.
Taarifa ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga imeweka wazi uzito wa changamoto hiyo kwa kuonyesha kuwa mwaka 2025 pekee kuliripotiwa matukio ya moto zaidi ya elfu tatu ambapo maisha ya watu 114 yalipotea huku mamia wengine wakijeruhiwa.



Post a Comment