Wasafi haiipingi Sheria ya Huduma za Habari, Diamond aipongeza JAB na kuiunga mkono Serikali
Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Wasafi Media, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, amesema wazi kuwa Wasafi Media haina msimamo wa kupinga Sheria ya Huduma za Habari, bali inaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini, akipongeza mchango wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) katika kuleta nidhamu na weledi kwenye sekta hiyo.
Diamond ameyasema hayo baada ya kufika katika Ofisi za JAB kwa lengo la kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusu utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari, akisisitiza kuwa vyombo vyake vipo tayari kutekeleza kikamilifu matakwa yote ya kisheria kwa watumishi wake.
Amesema Wasafi Media haitafuti njia za kukwepa Sheria, bali inalenga kushirikiana na Serikali na taasisi zake kuhakikisha taaluma ya habari inalindwa na kuendelezwa kwa misingi ya maadili, elimu na uwajibikaji.
Amebainisha kuwa licha ya Sheria hiyo kuathiri vyombo vya habari kwa namna moja au nyingine, haiwezi kupingwa kwa kuwa Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa wadau kujipanga na kutimiza vigezo vilivyowekwa, ikiwemo suala la waandishi kuwa na sifa stahiki za kitaaluma kuanzia ngazi ya Diploma na kuendelea.
Diamond amekiri kuwa kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati kumeleta mabadiliko chanya katika sekta ya habari, akisema kumeongeza nidhamu, uwajibikaji na uelewa wa wajibu wa kisheria kwa wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wenyewe.
“Sisi hatutaki kukwepa utekelezaji wa Sheria. Hakuna namna unaweza kuvunja Sheria na ukabaki salama. Wasafi tumehakikisha watumishi wetu wanazingatia Sheria, na katika hilo sina utani,” amesema Diamond.
Ameongeza kuwa awali alipokea taarifa na tafsiri tofauti kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, lakini baada ya kufika JAB na kupata ufafanuzi wa kina, ameielewa vyema dhamira ya Serikali ya kuijenga na kuilinda taaluma ya uandishi wa habari kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, amesema Sheria ya Huduma za Habari ilitungwa mwaka 2016 na Serikali ilitoa kipindi cha mpito cha miaka mitano, kikaongezwa miaka miwili, na baadaye kupita miaka mingine mitatu, hivyo kufikisha jumla ya miaka kumi.
Amesema Serikali inaamini kuwa muda huo ulikuwa wa kutosha kwa waandishi wa habari na wadau wote wa sekta hiyo kutimiza vigezo vya kisheria, hatua inayolenga kujenga taaluma ya habari yenye weledi, maadili na heshima kwa maslahi mapana ya Taifa.

Post a Comment