MOTSEPE AFUNGUKA SOKA LA AFRIKA KUCHAFULIWA, ACHUKUA HATUA




Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe, ameamua kuingia uwanjani mwenyewe akiwa na hasira baada ya matukio yasiyovumilika yaliyojiri kwenye fainali za AFCON 2025 kule Morocco. 

Dk Motsepe ameweka wazi kuwa hatamvumilia mtu yeyote anayejaribu kuchezea heshima, uaminifu na hadhi ya soka la Afrika.

Katika hotuba yake iliyotoka Ijumaa wiki hii, kupitia mtandao wa CAF bosi huyo amesema ameudhiwa  na "matukio" ya ajabu yaliyotokea Morocco na sasa ameamua kupiga filimbi ya mabadiliko makubwa ya kanuni ili kuadhibu vikali tabia zinazoharibu ladha ya mchezo.

Amri ya Kikosi cha EXCO 

Motsepe ametangaza kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya CAF (EXCO), ambayo ndiyo chombo chenye "mamlaka ya mwisho" nje ya Mkutano Mkuu. Lengo ni moja tu: Kuzifanyia upasuaji kanuni za nidhamu. 

Motsepe anataka vyombo vya kisheria vya CAF viwe na "nguvu ya ziada" ya kupiga rungu kwa yeyote anayekiuka sheria za soka la Afrika hadi ajute.

"Nimechukizwa sana na matukio ya hovyo yaliyotokea fainali za Morocco. Nimeyaona maamuzi ya Bodi ya Nidhamu yaliyotoka Jumatano ya Januari 28, 2026, na nayaheshimu, lakini sasa tunakwenda kubadilisha sheria ili kuwa na adhabu kali zaidi zinazotisha (dissuasive sanctions)," alisema Motsepe.

Mwamuzi Siyo Adui, Ni Fundi! 

Kwenye upande wa waamuzi, Motsepe amesema CAF inapanga kumwaga mpunga mrefu ili kuhakikisha waamuzi wa Afrika, waendesha VAR na makamishna wa mechi wanakuwa wa viwango vya utaalamu na maamuzi kwa kiwango cha dunia. Hataki kusikia malalamiko ya upendeleo au uwezo mdogo.

Amesisitiza kuwa tangu aingie madarakani, amehakikisha Kamati ya Waamuzi inakuwa huru na haifungamani na upande wowote. "Tunataka waamuzi wetu waheshimike duniani kote kama watu wa haki na wenye ujuzi wa hali ya juu," aliongeza.

Motsepe amewaambia mashabiki wa soka barani Afrika kuwa ana imani kubwa kuwa hatua hizi mpya zitafanya mashindano ya CAF yaendelee kuaminika, kupendwa na kuwa miongoni mwa mashindano bora zaidi duniani.


No comments