Bandari ya Pemba kufungua zaidi milango ya utalii




Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Pemba ina vivutio vingi vya utalii hivyo ujenzi wa Bandari ya Mkoani, Pemba itafungua zaidi milango katika sekta mbalimbali.

Mhe. Masauni amesema, Bandari ya Mkoani ni kiunganishi na muhimili wa maisha ya kila siku ya wananchi wa Pemba, ni lango la biashara, elimu, afya, utalii na mshikamano wa kijamii kati ya Pemba, Unguja na Tanzania Bara.



Ameyasema hayo Januari 10, 2026 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la kisasa la abiria katika bandari hiyo ambapo jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria zaidi ya 1,500 na kuinua huduma za bandari kwa viwango vya kimataifa, ikiwa ni shamrashara kuelekea miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya abiria wanaosafiri kwenda na kutoka Kisiwa cha Pemba hutumia usafiri wa baharini, hali inayoifanya bandari hiyo kuwa na umuhimu kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Usafiri wa baharini si mbadala, bali ni mahitaji muhimu ya maisha ya wananchi wetu, ndiyo maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeona umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, salama kwa abiria,” amesema Mhe. Masauni.



Amesema ujenzi wa jengo hilo unatokana na mkataba wa uwekezaji kati ya Shirika la Bandari na wawekezaji wa Fumba Port, akibainisha kuwa ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya kimkakati.

 “Ushirikiano huu unapunguza mzigo kwa Serikali, unaongeza ubora na ufanisi wa huduma, na kuchochea uchumi kupitia ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla,” amesema.

 Amewata watoa huduma wa bandari, waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa majini pamoja na abiria kuitumia miundombinu hiyo kwa nidhamu, uadilifu na kuitunza ili idumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo, wakandarasi na wasimamizi wa mradi kuhakikisha ujenzi unatekelezwa kwa ubora unaostahili, kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha. 

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa usafiri wa uhakika kwa abiria wanaosafiri kati ya Pemba, Unguja na Tanzania Bara. 



Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Pemba Mhe. Miza Hassan Faki, amesema uwepo wa bandari hiyo umechangia ongezeko la meli zinazotia nanga katika eneo hilo, akisema kuwa awali bandari ilikuwa inapokea abiria 60,000 kwa mwezi lakini kwa sasa inapokea zaidi ya abiria 100,000. 

Ameongeza kuwa bandari hiyo imechangia pia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo ya jirani, hususan vijana ikiwa pamoja na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mafuta ambapo awali uwezo wa kuhifadhi mafuta ulikuwa lita 100,000, lakini kwa sasa umeongezeka hadi kufikia lita milioni mbili.


 

 

No comments