MAAMUZI YA TRUMP: KUMBE HATA WAO WANAJUA UMUHIMU WA AMANI KWANZA



Katika muktadha wa matukio yanayoendelea Minnesota, uamuzi wa Rais Donald Trump wa kuweka jeshi tayari unaakisi falsafa ya utawala, inayosisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kila kitu. 

Mantiki inayotumika hapa ni kwamba haiwezekani kufanya mazungumzo yenye tija mitaani kukiwa na milipuko na uvunjifu mkubwa wa sheria kwani katika hali ya ghasia, hakuna upande unaoweza kumsikiliza mwingine. 

Rais Donald Trump amechukua hatua kali ya kuwaweka tayari wanajeshi zaidi ya 1,500 wa kikosi cha miamvuli kutoka kitengo cha 11 cha Airborne kwa ajili ya kuelekea Minnesota. Kikosi hiki ni kile chenye makazi yake Alaska, eneo lenye baridi kali kipindi chote cha mwaka.

Hatua hii inakuja kufuatia maandamano makubwa na ghasia zinazoendelea mjini Minneapolis, ambazo zimesababisha mivutano mikubwa kati ya raia na vyombo vya usalama.

Akizungumza kupitia jukwaa lake la Truth Social, Rais Trump amewashutumu wanasiasa wa Minnesota kwa kushindwa kudhibiti kile alichokiita "waasi wa kulipwa" na wachochezi wa kitaalamu. Trump amedai kuwa waandamanaji hao si raia wenye kero za kweli, bali ni watu waliopangwa kwa ajili ya kuwashambulia maofisa wa ICE ambao wanafanya kazi yao ya kusimamia sheria za uhamiaji.

Kutokana na hali hiyo, Trump ametishia kutumia sheria ya "Insurrection Act" ya mwaka 1807, inayompa Rais mamlaka ya kupeleka jeshi la nchi hiyo kupambana na uasi ndani ya ardhi ya Marekani. Amesema kuwa ikiwa viongozi wa jimbo hilo hawatawasimamisha waandamanaji hao, hatasita kuingilia kati ili kurejesha utulivu kama walivyofanya marais wengine waliotangulia katika historia ya nchi hiyo.

Kinadharia na kiutendaji Serikali zote huchukulia jukumu lake la kwanza kuwa ni kulinda maisha na mali, hivyo kuweka jeshi tayari ni hatua ya dharura ya kusimamisha mzozo usizidi kuwa mbaya ili kutengeneza mazingira yatakayoruhusu watu kukaa mezani baadaye.

Hatua hii pia inalenga kuzuia kile kinachoitwa maambukizi ya ghasia au "Domino Effect" ambapo serikali huogopa kuwa ikiwa Minneapolis itaonekana kushindikana, miji mingine inaweza kufuata mkondo huo. Kwa kutuma ujumbe wa nguvu ya kijeshi kupitia kikosi cha miamvuli cha 11th Airborne, Rais anajaribu kukata mzizi wa fujo mapema na kuonyesha kuwa mamlaka ya dola bado ipo imara na makundi ya waasi wa kulipwa yasiamini kuwa yanaweza kuishinda nguvu serikali.

Zaidi ya hayo, kuna mtazamo wa kisheria unaoeleza kuwa utulivu ni sharti la lazima ili haki iweze kupatikana, kwani haki haiwezi kutafutwa katika mahakama ambazo zimefungwa au mazingira yaliyotawaliwa na hofu. Ili uchunguzi wa kifo mathalani cha Renee Good ufanyike kwa weledi na amri za majaji zisikilizwe, lazima mji uwe na utulivu kwanza. 

Kwa hatua za Trump Serikali inajenga hoja kuwa inatengeneza mazingira ambapo sheria inaweza kupumua, ikiamini kuwa mashambulizi dhidi ya maofisa wa usalama yanamaanisha mfumo wa mazungumzo umeshaharibika na unahitaji kurejeshwa kwa nguvu.

Uamuzi huu wa kutumia nguvu kubwa, au "Hard Power," ni mbinu ya kutafuta utulivu wa muda ili kununua wakati wa kutumia diplomasia au "Soft Power" hapo baadaye. 

No comments