DC MPOGOLO AMALIZA MGOMO WA WAFANYAKAZI NAMERA

 


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amefanikiwa kumaliza mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 1,500 wa Kiwanda cha NAMERA kilichopo Gongolamboto jijini Dar es Salaam.

Mgomo uliokuwa umeanza tarehe 16 Januari 2026. 

Mgomo huo ulitokana na madai ya mishahara, ambapo mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi umewekwa kwa mujibu wa Tangazo na Amri ya Serikali Namba 605A ya tarehe 13 Oktoba, 2025, inayotoa ongezeko la wastani wa asilimia 33.4. Kutokana na amari hiyo, mshahara wa chini umeongezeka kutoka Shilingi 275,060 mwaka 2022 hadi Shilingi 358,222 mwaka 2025. 

Akizungumza na wafanyakazi pamoja na uongozi wa kiwanda hicho, Mhe. Mpogolo amesisitiza kuwa Amri ya Serikali ni ya lazima kutekelezwa na kwamba hakuna kampuni, taasisi au mwajiri yeyote anayekubalika kushuka chini ya viwango vilivyowekwa kisheria. Ameeleza kuwa makubaliano yoyote hayawezi kwenda kinyume na Amri ya Serikali.

Mpogolo ametoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda na wafanyakazi, ikiwemo kuhakikisha malipo ya mishahara yanatolewa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 605A la mwaka 2025, huku akisisitiza kuwa hakuna mfanyakazi atakayefukuzwa kutokana na kushiriki mgomo. 

Aidha, amekitaka kiwanda kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi (TUICO) na Afisa Kazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufanyika uchaguzi wa viongozi wa wafanyakazi watakao kuwa kiungo madhubuti kati ya wafanyakazi na uongozi, pamoja na kupitia mikataba ya ajira kuhakikisha inakidhi sheria na kanuni zinazohitajika. 

Mpogolo pia amehimiza ujenzi wa mahusiano mazuri na kulinda kiwanda kutokana na mchango wake mkubwa katika uchumi wa taifa na nafasi zake muhimu za ajira kwa wananchi.

Kwa upande wao, wafanyakazi wa kiwanda hicho wameeleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya, wakisema kuwa zimeleta matumaini mapya na kurejesha amani kazini. Wameahidi kurejea kazini mara moja na kuendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala (RPC), ACP Yustino Mgonja, amepongeza juhudi za Mhe. Mpogolo katika kushughulikia mgogoro huo kwa haraka na kwa busara. ACP Mgonja amesema hali ya usalama katika eneo la kiwanda ni shwari na amewahakikishia wafanyakazi kuwa wapo salama.

Kwa upande wake, mmiliki wa Kiwanda cha NAMERA,Muhammed Waseem amesema yupo tayari kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa kati ya uongozi wa kiwanda na Serikali, huku akiahidi kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha ushirikiano kati ya waajiri na wafanyakazi kwa maslahi ya pamoja.

Dc. Mpogolo amesema kuwa kiwanda hicho ni muhimu sana, hasa katika upande wa ajira. Hivyo basi, migogoro inaweza kuharibu upatikanaji wa ajira na ukuaji wa uchumi, kwa hivyo migogoro si jambo zuri.

Kufuatia kumalizika kwa mgomo huo, shughuli za uzalishaji katika Kiwanda cha NAMERA zinatarajiwa kurejea kama kawaida, huku wafanyakazi wakirejea kazini wakiwa na ari mpya ya kufanya kazi.

No comments