BFT YATANGAZA RASMI KALENDA YA MATUKIO YA VITASA
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) imetangaza rasmi kalenda ya matukio ya mwaka 2026 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha na kukuza mchezo wa ngumi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa BFT Makore Mashaga kalenda hiyo imetolewa baada ya kupitiwa na kamati katika kikao maalumu kilichofanyika Januari 21,2026.
Makore katika taarifa yake aliwataka wadau mbalimbali washirika, wafadhili, na taasisi mbalimbali kushirikiana na BFT katika kufanikisha utekelezaji wa matukio yote yaliyopangwa kwa mwaka huu. Kalenda hii inajumuisha mashindano ya kimataifa, kitaifa, kozi za mafunzo kwa makocha na waamuzi wa mchezo wa ngumi, pamoja na mikutano na vikao mbalimbali vya maendeleo ya ngumi nchini.
Makore alisema katika mashindano ya kimataifa, BFT imepanga kushiriki Mashindano ya Kanda ya 3 Afrika yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22 hadi 26 Aprili 2026. Aidha ratiba pia inaonyesha kuwepo kwa Mashindano ya Ubingwa wa Afrika nchini Zambia kati ya mwezi Mei na Juni, pamoja na ushiriki wa michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2026.
Kitaifa, mwaka utaanza kwa Mashindano ya Wazi ya Ubingwa wa Taifa kwa Wanawake yatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari 2026, yakifuatiwa na Mashindano ya Wazi ya Ubingwa wa Taifa kwa wanaume na wanawake yatakayofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 Machi 2026.
Shirikisho pia linatarajia kuzindua Ligi ya Ngumi ya BFT tarehe 23 Mei 2026 jijini Dar es Salaam kwa mtindo wa Pro Boxing, ikizishirikisha timu za Ngome na JKT pamoja na mabondia maarufu wa kitaifa na kimataifa. Mashindano mengine ni pamoja na Kombe la Taifa mkoani Dodoma kuanzia tarehe 9 hadi 13 Juni, Mashindano ya Klabu Bingwa ya Taifa mkoani Tanga tarehe 26 hadi 30 Agosti, na Mashindano ya Vijana jijini Dar es Salaam mwezi Septemba.
Kalenda itahitimishwa kwa Mashindano ya Kombe la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Mara kuanzia tarehe 10 hadi 14 Oktoba, na kufuatiwa na Mashindano ya Bingwa wa Mabingwa jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 25 hadi 28 Novemba 2026.
Kwa upande wa kuwajengea uwezo watendaji, BFT itafanya mfululizo wa kozi za waamuzi na makocha kuanzia daraja la kwanza hadi ngazi ya taifa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, na Mara kulingana na tarehe za mashindano yaliyopangwa. Kuhusu masuala ya utawala, Mkutano Mkuu wa mwaka 2025 umepangwa kufanyika tarehe 20 Aprili 2026, wakati Mkutano Mkuu wa mwaka 2026 utafanyika jijini Dodoma tarehe 12 Juni 2026.
Makore amesema kwamba BFT inawaalika wadau wote wa michezo, makampuni, na taasisi mbalimbali kujitokeza kushirikiana nayo kwani milango iko wazi katika maeneo yote yaliyopangwa kwa lengo la kufanikisha mwaka wa ngumi wa 2026.
Post a Comment