USANIFISHAJI WA SHULE SABA ZA MICHEZO WAKAMILIKA
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imekutana na Ujumbe wa Wakala wa Majengo Tanzania(TBA) kujadili kuhusu ujenzi wa Shule Saba za michezo nchini katika hatua ya usanifishaji na gharama za ujenzi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Desemba 11, Mtumba jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Methusela Ntonda amesema kuwa ujenzi wa Shule hizo saba ni mwanzo tu lakini Serikali imedhamiria kujenga Shule 56 za michezo nchi nzima.
"Tutajenga shule saba kwa hatua hii ya awali, lakini kadri bajeti itakavyoruhusu tutaongeza mpaka kufikia Shule 56 nchi nzima", alisema Ntonda.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Ujenzi Bi. Asnat Marero kutoka Wakala wa Majengo Tanzania(TBA) alisema kuwa miradi hii ina bajeti kubwa, hivyo katika Shule teule tutajenga Uwanja mmoja wa mpira wa miguu wenye eneo la kukimbilia, na Uwanja mmoja wenye matumizi mbalimbali.
Shule saba zitakazojengwa awamu ya kwanza ni Dodoma Secondary(Dodoma), Ikwiriri Secondary(Pwani), New Kiomboi(Singida), Dr. Damas Ndumbaro(Ruvuma), Bisheshe Secondary(Kagera), Nanguruwe(Mtwara), na Kicheba Secondary(Tanga).
Post a Comment