POLISI YAONYA WACHOCHEZI KUBADILI MBINU KILA MARA, YATAKA WANANCHI KUENDELEA KUKATAA VURUGU
Jeshi la Polisi
Tanzania limetoa wito kwa umma kuendelea kudumisha amani na utulivu, huku
likisisitiza kuwa linashuhudia juhudi za mara kwa mara za kubadilisha mbinu za
uchochezi zenye lengo la kuingiza vurugu na chuki nchini.
Taarifa
iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu, mjini Dodoma, David Misime
imesisitiza umuhimu wa kushirikiana na kukataa uchochezi huo.
“Tukatae yale
yote yanayohamasishwa kwa njia mbalimbali na katika maneno ya kubadilisha mbinu
kila mara ili kutaka kutuchonganisha na kutujengea chuki kati yetu.”
Taarifa
hiyo iliongeza kuwa lengo la vitendo hivyo vya uchochezi ni “kutuuingiza
katika vurugu ambazo matokeo yake siyo mazuri kama tunavyo shuhudia katika
maeneo mengine duniani.”
Hali ya Usalama Nchini Iko Shwari
Wito
huo wa Polisi unakuja siku moja baada ya kutoa taarifa ya kuhakikisha
Watanzania hali ya usalama. Jeshi la Polisi, kupitia taarifa yake,
limewajulisha wananchi kuwa, “kwa ushirikiano wa Vyombo vya Ulinzi na
Usalama pamoja na ninyi wananchi na wadau wengine katika kutimiza jukumu la
kulinda amani, utulivu na usalama nchini, hadi sasa nchi yetu kiusalama ni
shwari na shughuli za kiuchumi na za kijamii ziliendelea vizuri katika
mazingira ya amani kwa kipindi hicho cha masaa 24.”
Jeshi
hilo limeeleza kuwa wanapoendelea kuelekea siku ya mwisho wa wiki, wanatoa wito
kwa kila mmoja kuendelea kutii sheria, kushirikiana na kila mmoja na kutekeleza
wajibu wake katika kulinda na kuimarisha amani ambayo kila mmoja anaihitaji
katika maisha na shughuli zake za kila siku.
Jeshi
la Polisi limeahidi kuwa, kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na
Usalama, litaendelea kulinda usalama wa nchi yote, maisha na mali za kila
mmoja, pamoja na Taifa zima la Tanzania.

Post a Comment