RC TANGA NA MWANAFA WAKOSHWA NA HALE FESTIVAL
Mji wa Hale mwishoni mwa wiki uligubikwa na hisia za kipekee wakati bendi kongwe za Msondo Ngoma na Sikinde zilipotandika muziki wa dansi kumuenzi gwiji TX Moshi William. Tukio hilo ni sehemu ya msimu wa tatu wa Hale Festival, ulioratibiwa na Dkt. Hassan Abbas.
Akizungumza katika usiku maalum wa kumkumbuka gwiji la muziki wa dansi, marehemu TX Moshi William uliofanyika Hale Lounge, Balozi Batilda alisema tamasha hilo ni mfano wa kuigwa katika kuenzi tunu za sanaa. "Kupitia Hale Festival, tunaweza kupata akina TX Moshi wengi zaidi. Hongera Dkt. Abbas kwa maono haya," alisema.
Kwa upande wake, mwandaaji Dkt. Abbas—ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii—alisema tamasha hilo ni sehemu ya kumuishi TX Moshi, aliyeanza muziki mkoani humo kabla ya kuwa gwiji wa kitaifa.
Mbali na burudani, tamasha hilo limekuwa na tija kwa vijana kupitia mashindano ya soka ya Hale Cup. Meneja wa Msondo Ngoma, Said Kibiriti, alimshukuru Dkt. Abbas kwa kuenzi mchango wa TX Moshi, huku mtangazaji Zuber Zomboko akikabidhi nakala za nyimbo zote za marehemu kwa viongozi hao kama sehemu ya kumbukumbu ya kudumu.
Katika kilele cha tamasha hilo, Dkt. Abbas alimtunukia marehemu TX Moshi William Tuzo ya Heshima (Lifetime Achievement Award), iliyopokelewa na mwanawe, Hassan TX Moshi Jr.
Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), alipongeza hatua ya kuziunganisha bendi kongwe za Msondo Ngoma na Sikinde jukwaa moja. Katika kuunga mkono sanaa hiyo, RC Batilda na MwanaFA walichangia shilingi milioni 1.5 kila mmoja kwa bendi hizo.
Dkt. Abbas alibainisha kuwa msimu huu wa tatu wa tamasha hilo umeambatana na mashindano ya soka ya ‘Hale Cup’ yanayoshirikisha timu 24, huku fainali ikitarajiwa kupigwa Januari 1, 2026.




Post a Comment