AFCON 2025:DHORUBA YA SARE YAKUMBA VIGOGO, BENIN YAFUFUA MATUMAINI
Mzunguko wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) nchini Morocco umeshuhudia kimbunga cha sare kikizikumba timu vigogo, huku rekodi ya ushindi mfululizo ya wenyeji Morocco ikifikia tamati mbele ya Mali.
Wenyeji Morocco 'The Atlas Lions' wameshindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani wa Prince Moulay Abdellah baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mali katika Kundi A. Matokeo haya yamesitisha rekodi ya kuvutia ya Morocco ya kushinda mechi 18 mfululizo na kuwazuia kufuzu mapema hatua ya 16 bora.
Mchezo huo ulitawaliwa na matumizi ya Teknolojia ya Usaidizi wa Mwamuzi (VAR) ambapo penalti mbili ziliamuliwa kwa pande zote; Brahim Diaz aliiweka Morocco mbele, lakini Lassine Sinayoko akasawazisha kwa Mali. Kipa wa Mali anayekipiga nchini Tanzania (Yanga), Djigui Diarra, alikuwa nyota wa mchezo baada ya kuonyesha kiwango bora kwa kuokoa nafasi kadhaa za hatari.
Katika mchezo mwingine wa Kundi A, Comoro imeendelea kuonyesha upinzani kwa kutoka suluhu ya 0-0 na Zambia. Kwa sasa, Morocco inaendelea kuongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na Mali na Zambia wenye pointi mbili kila mmoja, huku Comoro ikiburuza mkia na pointi moja.
Hali haikuwa tofauti katika Kundi B, ambapo Zimbabwe walitoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Angola mjini Marrakesh. Wakati huohuo, miamba ya soka Afrika, Misri na Afrika Kusini, waligawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Adrar, Agadir.
Tofauti na mvua ya sare katika makundi mengine, Benin 'The Cheetahs' wamefanikiwa kupata ushindi wao wa kwanza katika michuano hiyo kwa kuifunga Botswana bao 1-0 mjini Rabat. Bao la ushindi lilifungwa na Yohan Roche dakika ya 28 baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Steve Mounie.
Ushindi huo unaiweka Benin katika nafasi ya tatu ya Kundi D ikiwa na pointi tatu. Kwa upande wa Botswana, hali imezidi kuwa mbaya baada ya kupoteza michezo yote miwili na kubaki mkiani mwa kundi hilo bila pointi.
Hatima ya Kundi A itajulikana Jumatatu ijayo ambapo wenyeji Morocco watashuka dimbani kumenyana na Zambia mjini Rabat, huku Mali wakihitaji ushindi dhidi ya Comoro ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Post a Comment