RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI, AMTHIBITISHA CHANG'A TMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi katika taasisi mbalimbali za serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari S. Machumu akimkariri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Mhe. Dkt. Rahma Salim Mahfoudh ameteuliwa kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani, akichukua nafasi ya Bw. Julian Banzi Raphael ambaye muda wake umemalizika.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Dkt. Ladislaus Benedict Chan'ga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa akikaimu nafasi hiyo. Aidha, Profesa Muhammad Bakari Kambi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, akichukua nafasi ya Dkt. Ellen Mkondya Senkoro ambaye amemaliza muda wake wa utumishi.
Uteuzi huo pia umemgusa Balozi Wilson Kajumula Masilingi ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (TEITI). Balozi Masilingi anachukua nafasi ya CPA Ludovick Utouh ambaye amemaliza muda wake katika nafasi hiyo.

Post a Comment