SAUTI ZA WANANCHI: "Amani ni Ngao Yetu, Mshikamano Ndiyo Silaha ya Maendeleo Baada ya Uchaguzi"
Viongozi wa kijamii, kidini, na kisekta wametoa wito mzito kwa Watanzania wote kudumisha amani na utulivu kama msingi mkuu wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha uchaguzi mkuu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamesisitiza kuwa umoja wa kitaifa ndiyo siri ya mafanikio ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya ya Mkuranga, Shukuru Ngweshani, ameeleza kuwa ili kudumisha amani, Watanzania wanapaswa kuaminiana bila kubaguana.
"Ili tudumishe amani tunapaswa kuaminiana bila kubaguana kwani watu watakaa pamoja na kufanya shughuli za maendeleo kwa pamoja. Utulivu na mshikamano ndiyo jadi ya nchi yetu, tushirikiane katika kuleta maendeleo," alisisitiza Ngweshani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa African Talent Forum (ATF), Rosemary Bujashi, amewataka wananchi kuitazama amani kama ngao kuu ya kujilinda dhidi ya watu wasioitakia mema nchi yetu. Amehimiza Watanzania kupuuza sauti za wale wanaojaribu kuwagawa.
"Amani ni ngao ya nchi yetu, tunapaswa kuitumia ili kujilinda na wale wasioitakia mema nchi yetu. Tuilinde amani kwa gharama yoyote. Tudumishe mshikamano wetu katika kujiletea maendeleo ya nchi yetu na tuachane na wale wanaotaka kutugawa," alisema Bujashi.
Naye Diwani wa Kata ya Mkuranga, Hamza Mahanaka, ametoa ujumbe mahususi kwa vijana akitaka waepuke makundi yanayoweza kuyumbisha uchumi na kurudisha nyuma juhudi za maendeleo. Amesema kuwa utulivu unatoa fursa kwa viongozi na wananchi kufanya kazi bila hofu huku ukivutia wawekezaji.
"Vijana tudumishe amani na kuachana na makundi ambayo yanarudisha nyuma juhudi za maendeleo na kuyumbisha nchi kiuchumi. Viongozi wahubiri upendo na mshikamano kuvutia wawekezaji... tuongeze mshikamano ili tuweze kujiletea maendeleo ya nchi yetu," alieleza Mahanaka.
Viongozi hawa wote wanagusia jambo moja kuu: Amani ya Tanzania ni tunu inayopaswa kulindwa na kila mzalendo. Baada ya uchaguzi, kazi iliyobaki ni moja tu—kushirikiana kama taifa moja kuelekea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Post a Comment