SAMIA AZIDI KUNYOSHA JIJI! DC Mpogolo Akagua Daraja la Sh Bilioni 7 Segerea
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na juhudi zake za dhati za kuleta maendeleo, ikiwemo kutoa fedha nyingi za ujenzi wa barabara katika Jiji la Dar es Salaam, hususan Wilaya ya Ilala.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, Awamu ya Pili (DMDP 2), Mpogolo alisisitiza kuwa Rais Samia ametoa zaidi ya Shilingi Bilioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo pekee.
"Natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye amelata fedha nyingi sana katika Wilaya yetu ya Ilala. Daraja hili peke yake linagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 7,” alisema Mpogolo wakati akikagua ujenzi wa Daraja la Majumba Sita-Segerea.
Sh 138,237,462,371.37 zimetengwa chini ya Mradi wa DMDP 2 kutengeneza jumla ya barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 146.06 katika mikataba mitano inayoendelea kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Miradi inayotekelezwa inajumuisha ujenzi wa barabara za katikati ya jiji zenye zaidi ya kilometa 15, pamoja na barabara za Banana - Kitunda – Kivule Msongola na Kivule - Majohe Njia Nne.
Pia, kuna ujenzi wa barabara za Migombani - Kiwalani, Banana - Kitunda, Baracuda - Chang'ombe - Majichumvi, barabara na Daraja la Majumba Sita - Segerea na Barabara ya Tabata - Maweni - Kisiwani.
Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ni pamoja na Jiangxi Geo Engineering Corp Ltd., ambapo Han Zhenliangni Meneja Mradi kwa Mkandarasi wa Kivule na Wang Qingyong ni Meneja Mradi wa Segerea - Majumba Sita.
Alisema Daraja la Segerea - Majumba Sita ambalo ni muhimu kwa sababu linaunganisha Kata za Kiwalani na Segerea na muhimu kwa shughuli za kiuchumi na mahusiano ya kijamii linagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 7 na litakuwa na urefu wa zaidi ya meta 80 na ujenzi upo katika hatua za kuweka nguzo.
Kati ya nguzo 54 zinazotarajiwa kujengwa, tayari wameshafikisha nguzo 27 Mkandarasi Jiangxi Geo Engineering Corp Ltd., aliyewakilishwa na Meneja Wang, alisema wanatarajia kukamilisha kazi zote za uwekaji nguzo mwishoni mwa mwezi huu ili kuanza ujenzi wa msingi wa daraja kabla ya msimu wa mvua kuanza.
Alisema utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia asilimia tano na kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza mzunguko mrefu ambao wananchi hulazimika kuufanya wakati mto unapojaa maji, hivyo kuokoa muda na kupunguza uchovu.
"Daraja hili ni muhimu sana kwa watu wa Jimbo la Segerea, kiunganishi cha Kata ya Kiwalani na Segerea. Ni daraja ambalo lina umuhimu mkubwa kwa shughuli za kiuchumi," alisisitiza Mpogolo.
Post a Comment