JKT Queens yalala 4-1 kwa TP Mazembe

Stumai Athumani akishangilia baada ya kufunga goli katika dakika ya 12,

Mabingwa watetezi TP Mazembe wamekata tiketi ya  nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF 2025 baada ya  kuwafunga JKT Queens ya Tanzania kwa mabao 4–1 katika mechi ya mwisho ya Kundi B.

Ushindi huo unaendeleza rekodi ya Mazembe dhidi ya timu zinazoingia mashindanoni kwa mara ya kwanza na unahakikisha kwamba mabingwa hao watetezi wanasalia kwenye mbio za kutetea taji lao wakati hatua ya mtoano itakapoanza wiki ijayo.

Katika mchezo huo JKT walitangulia kupata bao kupitia kwa Stumai Athumani katika dakika ya 12, lakini majibu ya Mazembe yalikuwa ya haraka na ya kinyama.

Marlene Yav Kasaj alisawazisha kwa penalti katika dakika ya 23 kabla ya mchezaji wa kimataifa wa Nigeria, Oluwayemis Samuel kumalizia mpira vyema dakika sita baadaye (29').

Kabla  ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza, mchezaji wa Ghana, Grace Acheampong, aliipatia timu yake goli la tatui  (45+3’) na kuwapa mabingwa hao udhibiti kamili wa mchezo.

Goli la kusawazisha la Marlene Yav Kasaj 

Kipindi cha pili TP Mazembe walicheza kwa akili na dakika ya 66 Yav Kasaj alifunga goli la nne kwa penalti .

Ingawa JKT walijisukuma kutafuta njia ya kurudi mchezoni lakini hawakuweza kuivuruga safu ya ulinzi ya Wakongo iliyojipanga vyema.

Matokeo hayo yanaipandisha Mazembe hadi alama sita na nafasi ya pili katika Kundi B, na kuwapeleka nusu fainali nyuma ya washindi wa kundi hilo, ASEC Mimosas (alama saba), ambao waliwafunga Gaborone United 4–0 katika mechi nyingine ya siku hiyo.


JKT Queens wanamaliza wakiwa wa tatu kwa alama mbili, huku Gaborone wakiwa wa nne.

Mazembe sasa wanaelekeza nguvu zao katika nusu fainali huku wakifukuzia kurejea fainali, wakati JKT Queens wameondoka huku wakiwa wameonyesha ishara za maendeleo dhidi ya wapinzani wakubwa.

No comments