Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, July 16, 2024

Majaliwa azindua VAR, vifaa vya matangazo Azam

 



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uzinduzi wa vifaa vya kisasa vya kurushia matangazo ya mpira wa miguu na video za usaidizi wa waamuzi (VAR) vitasaidia kuleta mashindano mengi ya kimataifa nchini.

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa vifaa hivyo vya Azam Media uliofanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jana.

“Azam Media mmetupeleka kwenye vigezo vya Afcon kuchezwa Tanzania, kutokana na ubora wa vifaa vyenu na huu uzinduzi wa VAR,” alisema Majaliwa.

Alisema VAR itasaidia kuondoa malalamiko kwa timu pamoja na kupunguza makosa ya kibinadamu kwa waamuzi na kuwa makini katika kazi zao.

Vilevile alisema soka la Tanzania limeendelea kukua kwa sababu ya maboresho ya miundombinu kwa sekta zote ikiwemo Azam Media kwa kuleta mitambo imara ambayo itawezesha soka letu kuonekana sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi.

“Kazi iliyopo TFF ni kuwapa masharti wamiliki wa viwanja, asiyetimiza awekwe pembeni. Tunahitaji kufika mbali kwenye viwango vya Afrika baada ya namba sita basi tuwe namba nne au mbili, ili tukapambane na Morocco na Misri,” alisema Majaliwa.

Vilevile alisema serikali itatimiza ahadi ya waziri aliyepita katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa juu ya kuleta VAR kama ilivyoahidiwa.

Aidha, alisema serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeingia kwenye sekta ya michezo na kutoa hamasa mbalimbali kwenye michezo ikiwemo goli la mama ambalo limeongeza hamasa kwa timu kufanya viuri kwenye michuano ya kimataifa.

“Rais amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha kwa kutoa goli la mama kwa timu za taifa hata klabu ambazo zitashiriki michuano ya kimataifa,” alisema Majaliwa.

Vilevile alisema Tanzania kuwa mwenyeji michuano ya Afcon 2027 ni jitihada za Rais Samia kwa ushirikiano na wenzake wa Kenya na Uganda, William Ruto na Yoweri Museveni.

No comments:

Post a Comment