Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepokea
kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa ya kifo cha shabiki maarufu wa
Young Africans, Ally Mohammed anayefahamika zaidi kwa jina la Ally
Yanga, kilichotokea jana Jumanne Juni 20, 2017 kwa ajali ya gari
iliyotokea mkoani Dodoma.
Katika
salamu za rambirambi kwa uongozi wa Young Africans, familia, ndugu,
jamaa na marafiki wa marehemu Ally Yanga ambako Rais Malinzi amewaasa
kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwao na kwa huzuni
amewafariji akisema: “Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake
tutarejea.”
“Hakika
nimeshtushwa na taarifa za kifo cha Ally Yanga ambaye nimejulishwa kuwa
kilitokea katika ajali ya gari huko Dodoma. Kifo hiki kimefanya
wanafamilia wa mpira wa miguu kupoteza hazina ya hamasa popote pale
uwanjani,” amesema Rais Malinzi.
“Binafsi
nilimjua Ally Yanga katika masuala ya mpira wa miguu hasa akishabikia
Young Africans na timu zote za taifa bila kujali kuwa ni Twiga Stars
(Timu ya taifa ya wanawake), Taifa Stars, Serengeti Boys au ile
Ngorongoro Heroes,” amesema Malinzi.
“Hivyo,
nawatumia Young Africans salamu zangu za rambirambi nikiwapa pole kwa
kuondokewa na mmoja wa mashabiki mwenye mvuto wa kipekee katika hamasa
uwanjani, lakini pia alikuwa akisapoti timu za taifa,” amesema Rais
Malinzi.
Aidha,
Malinzi amesema: “Nawatumia pole wanachama wote wa Young Africans kwa
kuondokewa na Shabiki mahiri Ally Yanga. Nawapa pole pia familia, ndugu,
jamaa na marafiki ambao wamepoteza mhimili wao.
“Naungana
nao katika msiba huu ambao pia ni msiba wetu sote wanafamilia ya mpira
wa miguu. Naungana nao pia kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya
Marehemu Ally Yanga. Amina.”
No comments:
Post a Comment