BARAZA la
Michezo Tanzania (BMT), limebariki kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mkoani
Dodoma.
Akizungumza
na wandishi wa habari leo Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema BMT
wameitakia uchaguzi mwema wenye amani, upendo na utulivu lakini TFF wameagizwa
kupitia sheria za Baraza la Michezo, Kanuni za Baraza na kanuni za Usajili,
hususani kanuni ya 8 (1) na (2).
“BMT wameitakia
TFF uchaguzi mwema wenye amani, upendo na utulivu lakini pia wameagiza TFF
kuwaeleza wagombea wote utii wa sheria na kuepuka kushika nyadhifa mbili kwa
wakati mmoja,” alisema Lucas.
Pia BMT
imesema Kanuni ya 8 (1) na (2), inaagiza
kuwa endapo wagombea wote watakaoshinda nafasi wanazowania kwa sasa ndani ya
TFF, hawana budi kuachia nafasi mojawapo katika uongozi wa mpira kwa miguu
katika ngazi ya wilaya au mkoa aliyoshinda awali.
Katika barua
yake iliyoandikwa Juni 19, mwaka huu na kusainiwa na Katibu Mkuu wa BMT,
Mohammed Kiganja, Baraza hilo limesema: “Uchaguzi huu usivuruge amani iliyopo
nchini na wagombea wakumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.”
Aidha Baraza
limesisitiza kuwepo na haki katika mchakato mzima kuelekea kwenye uchaguzi na
mchakato wake uwe huru na amani na usiwe ni kichocheo cha uvunjifu wa amani.
“Baada ya
viongozi kupatikana, watakula kiapo cha utii, na kujaza fomu Namba 5 ya BMT ya
utekelezaji majukumu yao kama Kanuni ya 8 (4) inavyoeleza,” alisema Kiganja.
Kadhalika,
mara baada ya uchaguzi, Baraza limeagiza kuhusisha baadhi ya vifungu vya sheria
ya Baraza ili viendane na katiba za TFF na wadau pamoja na kanuni zao.
No comments:
Post a Comment