WAGOMBEA 74 wamechukua
na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 12,
mwaka huu.
Hadi zoezi
hilo linafungwa jana saa 10.00 jioni wagombea wote wamerejesha, kwenye nafasi
ya urais, jumla ya wagombea 10 walijitokeza kuomba nafasi hiyo wakati kwenye
makamu rais wamejitokeza sita.
Akizungumza
na gazeti hili Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema 58 wamejitokeza
kuwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji katika Kanda mbalimbali.
“Zoezi la
kuchukua na kurejesha fomu kwa mujibu wa Kanuni ya 10, limefanyika kwa siku
tano kuanzia Juni 16, 2017 hadi Juni 20, mwaka huu na jumla ya wagombea 74 wamechukua na kurudisha fomu,”
alisema Lucas.
Siku ya
kwanza kuanza kutolewa fomu, Jamal Malinzi alikuwa wa kwanza kuchukua fomu akifuatiwa
na Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Athumani Nyamlani, Fredrick
Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.
Waliojitokeza
kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu ni Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura,
Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
Wajumbe wa
Kamati ya Utendaji kwa kufuata Kanda 13, Kagera na Geita wapo wanne, Mara na
Mwanza wanne, Shinyanga na Simiyu watatu, Arusha na Manyara watatu, Kigoma na
Tabora wanne.
Katavi na
Rukwa wawili, Mbeya, Songwe na Iringa wanne, Njombe na Ruvuma wanne, Lindi na
Mtwara wanne, Dodoma na Singida sita, Pwani na Morogoro wanne, Kilimanjaro na
Tanga watatu na Dar es Salaam wapo 15.
Kwa mujibu
wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, msomi Wakili Revocatus Kuuli alisema
mchujo utaanza leo hadi Juni 23, kwa mujibu wa kanuni ya 11.1 ya Uchaguzi wa
TFF na itafanywa na kamati ya Uchaguzi kwa wote waliojitokeza kuwania nafasi
mbalimbali kama inavyojionesha hapo juu.
”Mchujo
utafanyika (kesho) leo na wagombea na kuwaandikia barua za kuwajulisha juu
mchujo wa awali na Juni 24-25 tutachapisha na kubandika orodha ya awali ya
wagombea,” alisema Kuuli.
Kipindi cha
kuweka pingamizi ni Juni 26-28 na pingamizi zinatakiwa kuwekwa na wagombea
pekee na Juni 29 hadi Julai Mosi kupitia
pingamizi zote kufanya usaili wa wagombea.
Alisema
kamati ya uchaguzi itatangaza matokeo ya awali ya usaili Julai 2-3 na sekretarieti
itawasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya maadili Julai 4-6.
Wagombea
watakuwa na fursa ya kukata rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye
kamati ya rufaa ya maadili ya TFF baada ya kamati ya maadaili kutangaza matokeo
ya maamuzi ya kamati hiyo Julai 15-17.
Kipindi cha
kusikilizwa na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, Julai 29 hadi Agosti 4 na
orodha ya mwisho ya wagombea na kutangazwa Agosti 5-8 na kampeni kwa wagombea
wote itaanza Agosti 7-11
Uchaguzi
Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment