Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, February 14, 2014

TFF YAMWAGA VIFAA VYA LIGI MAALUM KWA AJILI YA KUBORESHA TIMU YA TAIFA




Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Jamali Malinzi, (kushoto) akimkabidhi Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Msanifu Kondo (kulia) jezi kwa ajili ya Ligi ya Taifa inayotarajiwa kuanza Februari 22, mwaka huu katika kanda tisa



MASHINDANO maalumu ya mikoa ya kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 22 hadi Machi 5 mwaka huu, huku ikiigharimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) takribani Sh. Milioni 360.

Michuano hiyo maalumu itashirikisha mikoa wanachama ya TFF na itakuwa ikichezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa timu mbili za kanda moja kuchuana na inatarajiwa kutoa wachezaji bora 60 wataoweka kambi ya siku 30 Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuuunda upya kikosi bora cha Stars, ili kiweze kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.

Malinzi alisema jumla ya timu 32 za Tanzania nzima zitashiriki michuano hiyo, kila mechi moja watakuwepo wasaka vipaji watano ‘Scouts’ kwa ajili ya kumulika wachezaji bora, pia mechi zote zitakuwa zikirekodiwa.

Baada ya zoezi la kuibua vipaji kwenye michuano hiyo, wasaka vipaji wote watajifungia (retreat) kwa muda wiki moja mjini Lushoto, Tanga kupitia rekodi zote za mechi na kuchagua wachezaji 60 bora, ambao watapelekwa Tukuyu, Mbeya kwa ajili ya mazoezi makali na wataalamu mbalimbali.
Wachezaji hao 60 watachujwa baada ya mwezi mmoja na kubaki 30, ambao watachanganywa na wachezaji wa sasa wa Taifa Stars na baadaye kupatikana kikosi bora kwa ajili ya mapambano ya kuwania kufuzu kwa AFCON.

Malinzi alisema wachezaji wa sasa wa Stars nao watakwenda kwenye kambi hiyo mkoani Mbeya mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mwezi Aprili.

“Tunaamini mfumo huo utasaidia kupata vijana wapya wa kuboresha kikosi cha Stars, hatutachagua majina wala kuangalia umri kwa kuwa hiki ni kipindi cha mpito na ni muda mchache umebakia kuelekea kwenye michuano hiyo,” alisema Malinzi.

Machi 5 mwaka huu Stars itashuka dimbani kuumana na Namibia katika mechi ya kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

No comments:

Post a Comment