Nguvu ya Kidijitali na Uzalendo: Kwa Nini Watanzania Tunapaswa Kumlinda na Kumbeba Latricia Kileleni
Katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi, ushindani wa urembo na tuzo za kimataifa kama Miss World umebadilika kutoka kuwa mashindano ya kawaida ya jukwaani na kugeuka kuwa vita ya ushawishi wa kidijitali na nguvu ya nchi husika mitandaoni.
Tanzania imepata fursa ya kipekee ya kusimama kwenye ramani ya kimataifa kupitia mwakilishi wetu Latricia, ambaye anawania Tuzo ya Multimedia (Multimedia Award). Hata hivyo, mafanikio katika nyanja hii hayaletwi tu na uzuri au utayari wa mshiriki mwenyewe, bali yanategemea kwa kiasi kikubwa namna nchi yake inavyosimama nyuma yake kama ngao na ngome ya kwanza ya ushindi.
Nguvu ya Kila Mwenye Simu
Tukiangalia takwimu za ukuaji wa matumizi ya simu za mkononi na upatikanaji wa intaneti nchini, tuna rasilimali kubwa isiyokadirika ya watu. Kila Mtanzania mwenye simu janja (smartphone) na line ya simu ana uwezo wa kubadilisha historia ya mashindano haya kwa sekunde chache tu kupitia kupakua App ya Miss World na kufuata taratibu zote za msingi za kumuunga mkono.
Upenyaji wa intaneti (internet penetration) nchini unatoa fursa kwa mamia na maelfu ya vijana na wananchi kuunganisha nguvu kwa pamoja. Kama nchi zingine zinavyofanya kwa kuhamasishana mpaka kufikia hatua ya kuona washiriki wao ni ajenda ya kitaifa, nasi tunapaswa kuiona safari ya Latricia kama ajenda yetu ya pamoja ya kizalendo.
Umuhimu wa Kuwa Sehemu ya Mchakato
Katika mataifa mengine duniani, ushiriki wa mrembo wao unachukuliwa kama suala la kiburi cha kitaifa (national pride). Wenzetu hawamsubiri mshiriki apambane peke yake; wanajipanga kimkakati kama jeshi la kidijitali kuhakikisha kila chapisho linapata alama za juu (engagement).
Ukweli ni kwamba tuzo za multimedia zinapimwa kwa nguvu ya jamii ya mtandaoni—kama vile kulike, ku-comment, ku-share, na kufuatilia akaunti za mshiriki. Hii inamaanisha kuwa ushindi wa Latricia upo mikononi mwetu asilimia mia moja. Kila kura tunayopiga na kila foleni ya kidijitali tunayounda kwa kum-follow na kuingia kwenye 'Community' ya Tanzania ndani ya app hiyo inamuongezea pointi za ushindi zitakazomweka mbali na washindani wake.
Wajibu Wetu Kama Taifa
Tukiwa kama wadau wa habari, burudani, na maendeleo ya kijamii, ni lazima tutambue kuwa ushindi wa kimataifa unakuza pia taswira ya nchi yetu na kuvutia ulimwengu kuangazia vipaji na utamaduni wa Tanzania.
Kumuunga mkono Latricia si suala la hiari pekee, bali ni wajibu wa kimkakati wa kuonesha utayari wetu wa kusimama na wawakilishi wetu kwenye majukwaa makubwa ya kimataifa. Wakati ukifika wa Septemba 5, ushindi hautakuwa wa Latricia peke yake, bali utakuwa ushindi wa kila Mtanzania aliyetoa dakika chache za muda wake kushusha App, kutoa kura, na kusambaza upendo kwa mrembo huyu anayepeperusha bendera yetu kwa fahari.


Post a Comment