LONDON, England
KATIKA karne ya 21, kumetokea
vituko vingi sana Ligi Kuu England, na hakika vimeleta mshangao kwa mashabiki,
viongozi, wanazi wa soka na wengine. Kwa ufupi hapa tunakuletea wachezaji
watano wanaotajwa ni wakorofi zaidi walioshangaza ulimwengu wa soka.
5. Lee Bowyer
Huyu
alianza soka kwa kuichezea timu ya Leeds United, iliyotamba enzi zake, kabla ya
kujiunga na Newcastle United na kumalizia soka lake West Ham United, zote za
England. Utata wa Bowyer ulianzia Charlton,
ambapo yeye na wachezaji wenzake walitajwa kuwa wavuta bangi sugu.
Utata
zaidi ulikuja baada ya kufukuzwa katika timu ya Leeds. Kwanza, Bowyer
alituhumiwa kwa ubaguzi akiwa kwenye maduka ya McDonalds, kisha mchezaji
mwenzake, Jonathan Woodgate alipewa adhabu baada ya kusababisha ajali nje
kidogo ya mji wa Leeds, katika klabu ya usiku.
Kesi
hiyo ilimgusa moja kwa moja Bowyer, ndipo uongozi wa Leeds United ukaamua
kumfukuza. Bowyer aliwahi kuzipiga kavu kavu na mchezaji mwenzake, Kieron Dyer,
na baadaye akafungiwa mechi 6, huku Jeshi la Polisi likimkamata kwa ukorofi.
Katika maisha yake ya soka alipewa kadi za njano 80 na kadi nyekundu 5 na
alijulikana kwa kukunjana ngumi na wachezaji mbalimbali kwenye mechi za Ligi Kuu
England.
4. Ashley Cole
Beki
mahiri wa kushoto aliyeanzia soka lake Arsenal na baadaye akajiunga na Chelsea,
ambayo anaichezea mpaka sasa. Hivi karibuni Cole ameichezea timu ya taifa ya
England mechi 100 na alipewa unahodha siku ya mchezo huo na mingine mara kadhaa.
Soka
lake lilianzia Arsenal, na alikulia kwenye timu hiyo akawa mchezaji muhimu wa
Arsene Wenger. Lakini maisha yake ya soka awali yalikuwa ni kuwadanganya
waamuzi kwa kujirusha kila alipokabiliana na wapinzani wake.
Akiwa
ndiye staa wa timu hiyo, aligundulika kuongea na kocha Jose Mourinho, aliyekuwa
akifundisha Chelsea. Cole ni mtata, kwa sababu aliwahi kusema haipendi nchi
yake ya England, na hataki hata kuishi nchi hiyo.
Alipopewa
ofa ya mshahara wa pauni 55,000 kwa wiki, alikataa mara moja na kuichanganya
Arsenal. Cole aliwahi kumdunda mwamuzi Mike Riley wakati alipotaka kumpa kadi
kwenye mchezo dhidi ya Hotspurs. Mwaka 2012 alikitukana Chama cha Soka cha
England, FA kwa kuwaita kundi la wapumbavu.
3. Eric Cantona
Staa
aliyetisha sana kwenye Uwanja wa Old Trafford, lakini anakumbukwa kwa utata
mwingi aliowaachia mashabiki wa England. Akiwa England, aliichezea Manchester
United, akiwa ni raia wa Ufaransa. Cantona si staa tu wa Man United, pengine
anakuwa mchezaji mwenye sifa nyingi kuliko wote waliowahi kucheza ligi kuu
England.
Lakini
mashabiki wa timu pinzani hawakumpenda kabisa, sababu alikuwa mtata sana kwenye
maamuzi yake. Cantona aliwahi kukwaruzana mara nyingi na mashabiki wa Leeds
United kwenye uwanja wa Elland Road.
Pia
anakumbukwa kwa kumpiga mateke shabiki wa Crystal Palace, hali iliyozidisha
ukorofi wake. Baada ya kung-fu hiyo, FA ilimfungia kutocheza soka miezi 9.
Licha ya kuchukiwa, Cantona aliisaidia Man United kutwaa mataji manne ya Ligi
kuu, mawili ya FA na Kombe la Ligi.
2. Luis Suarez
Staa
wa timu ya Liverpool, mzaliwa wa Uruguay. Ana kipaji kizuri cha soka, lakini ni
mtata kupindukia tangu akiwa ligi kuu Uholanzi. Kabla ya kuzua utata wake
Liverpool, alifanya hivyo akiwa na timu yake ya Ajax, aliwahi kumng’ata meno
mchezaji wa PSV na kufungiwa mechi 7.
Mwaka 2010 kwenye fainali za kombe la dunia,
Afrika Kusini, alizuia mpira uliokuwa ukieleka wavuni ambao ungeipa ushindi
Ghana na kusonga mbele, lakini ni Uruguay ilifanikiwa kutinga nusu fainali.
Licha
ya utata, Suarez aliifungia Liverpool mabao 30 msimu uliopita katika mashindano
yote.
Mwaka 2011 alikuwa na utata baada ya kumbagua beki wa Man United, Patrice
Evra na kufungiwa mechi nane. Baada ya kukataa kumpa mkono Evra msimu uliopita,
alifungiwa kwa kumng’ata mkono Branislav Ivanovic katika mchezo wa timu yake
dhidi ya Chelsea na kufungiwa mechi 12, ambapo amemaliza.
1.
Mario Balotelli
Alikuwa
mchezaji wa Manchester City, ambako alijiunga akitokea Inter Milan. Mkorofi
kweli huyu, sijui tutaanza na tukio gani kukumbuka wakati wake akiwa Etihad.
Alianza utata wake kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Manchester United, ambapo
timu yake ilishinda mabao 6-1.
Pambano
hilo la watani wa jadi lilimshuhudia Balotelli akishangilia bao kwa kuonyesha
fulana yenye maandishi “Why Always Me?” Baadaye katika mchezo muhimu wa kuamua
bingwa wa ligi kuu England dhidi ya Tottenham Hotspurs, Balotelli alimpiga
kichwa kiungo wa Spurs, Scot Parker.
Lakini
jambo zuri kwenye mchezo huo alifunga bao kwa njia ya penalti, ambalo liliipa
timu yake matumaini ya ubingwa. Pia aliwahi kugombana na Kolo Toure, pamoja na
aliyekuwa kocha wake, Roberto Mancini. Januari mwaka huu alijiunga na AC Milan,
lakini ligi kuu England haitamsahau nyota huyo.
No comments:
Post a Comment