DC MPOGOLO AZUNGUMZIA USAFI KAMA KINGA YA MWANZO DHIDI YA MAGONJWA



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo,  amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya hautakuwa na tija ikiwa wananchi hawatazingatia usafi wa mazingira wanayoishi na kufanyia kazi, kwani afya bora huanzia kwenye kinga na usafi ukiwa nguzo muhimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa. 

Mpogolo amesema hayo leo Julai 25, 2026, wakati wa zoezi la usafi wa mazingira linalofanyika kila Jumamosi asubuhi.

Mkuu huyo wa wilaya amesema zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuboresha huduma za afya kupitia ujenzi na uimarishaji wa vituo vya afya, zahanati na hospitali nchini.

Aidha Mhe. Mpogolo amewataka wafanyabiashara wote jijini Dar es Salaam kudumisha usafi katika maeneo yao ya biashara kila wakati, hususan siku za Jumamosi, na kuyataka makampuni ya ukandarasi wa usafi kutekeleza wajibu wao kwa kuondoa taka kwa wakati ili kuepusha mrundikano mbele ya maduka na maeneo ya biashara.

Akishiriki kikamilifu katika zoezi hilo ikiwa na pamoja na kusukuma mkokoteni wa taka mkuu huyo wa wilaya pia aliwapongeza madiwani, wenyeviti wa mitaa, watendaji, kampuni za usafi za SATEKI na Juza, pamoja na wananchi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha zoezi la usafi wa mazingira.

DC amemshukuru Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na makampuni yaliyochangia magari na vifaa vya kisasa vya usafi akisema mchango huo unaunga mkono juhudi za Serikali za kufanya Jiji la Dar es Salaam kuwa safi na salama.Pia amewashukuru wenyeviti wa mitaa kwa kujitolea kwao na kuomba mitaa yote katika Jiji la Dar es Salaam kuiga mfano wa Jangwani kwa ushirikiano waliouonesha katika kuhakikisha mazingira ya kata yao yanakuwa safi. 

Aidha, amezipongeza klabu za mpira na kampuni za usafi kwa kushiriki kusafisha eneo la Klabu ya Yanga Jangwani, huku akitoa wito kwa viongozi na wananchi wanaozunguka eneo la Klabu ya Simba kujiandaa kushiriki zoezi la usafi litakalofanyika wiki ijayo katika Barabara ya Msimbazi na maeneo yanayoizunguka klabu hiyo kama maandalizi ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi.

Vilevile, Ameongeza kuwa Halmashauri imepata tingatinga ambalo litatumika katika dampo kuu la Pugu ili kurahisisha shughuli za uondoaji na usimamizi wa taka.

No comments