Si vibaya,
wakati mwingine mtu ukaamua kuishi kama ndege. Maisha hayana maana wakati
mwingine, kama tu ukiwa huna maana na maisha yenyewe. Ni bora ukaishi kama
ndege tu. Ukiamua kuimba, imba, tena imba kwa sauti bila kujali watu
watasikiaje au watajali vipi. Maisha yanakuhitaji mwenyewe kwanza.
Zlatan
Ibrahimovic! Hana tofauti na ndege, anaimba sana. Nyimbo zake ni nzuri sana
masikioni mwake. Haijalishi mtu mwingine
atasikiaje. Na kwanini apoteze muda kujali hilo? Neno lake ni bora sana katika
moyo wake. Hawezi kunyamaza, hawezi kustahamili, ataongea tu. Na ataongea kwa
sauti, hajali ni nani atakwenda kulisikiliza.
Ana miaka 32
sasa, kichwani mwake anaamini yeye ni mchezaji bora sana duniani, hakuna kama
yeye. Anaamini pia, mkewe, Helena Seger, ni mwanamke mzuri sana
duniani, pengine kuliko wanawake wote unaoweza ukawadhania. Kila kitu bora na
kizuri katika dunia hii, basi ni lazima kiwe kinamzunguka yeye tu.
Huyo ndiye Zlatan Ibrahimovic ‘ Ibra Cadabra’. Mfalme wa soka kule nchini Sweden. Anajipenda
sana, anapenda kujiongelea yeye tu, na haijalishi kwa ukubwa gani. Ndiyo tabia
yake, siyo kosa lake pia! Huenda ndivyo alivyoumbwa hivyo.
John Carew, yule mtu mrefu ambaye kwenye ile miaka ya 2000 hadi 2004
alikuwa miongoni mwa watu walioing’arisha sana Valencia wakati ule. Ukiikumbuka
Valencia ya wakati ule, basi utayakumbuka vyema yale mabao hodari ya vichwa
yaliyokuwa yakifungwa na John Carew. Msimu uliopita alionekana akiwa na jezi ya
West ham. Hayupo kama zamani, lakini bado anaendelea kuitwa John Carew.
John Carew,
kwa bahati mbaya sana hamuelewi Ibrahimovic. Hamuelewi kabisa. Hauelewi uchezaji wake, haelewi pia kwa nini ‘Ibra Cadabra’ anajiingiza katika
kundi la wachezaji bora duniani. Ni kawaida kwa wachezaji kuwaziana hivi.
Lakini Ibra alijibu kwa wepesi sana, kuwa alichokuwa akikifanya Carew akiwa na
mpira, yeye anaweza kukifanya akiwa na chungwa. Hapa unahitaji akili kiasi
kujua Ibra alikuwa anamaanisha nini kwa Carew. Dharau iliyoje hiyo!!
Hampendi
Lionel Messi, hampendi sana Pep Guardiola, haipendi kabisa Barcelona.
Hawakumjali, hawakumthamini, alipuuzwa. Anajijua yeye ni mkubwa sana. Anapenda
iwe hivyo, siku zote tena kwa mtu yeyote.
Vipi Barcelona wampuuze? Anawachukia. Aliwahi kukaririwa akisema kuwa yeye ni
sawa na gari ya Ferrari, lakini Barcelona walimtumia kama Fiat.
Zlatan
anajijali sana, hajawahi kuamini kama kuna kitu kinapungua katika maisha yake.
Pamoja na uchezaji wake wote, hajawahi kuwa na wakala. Anaamini mawakala siku
zote wapo kwa ajili ya kumfanya mchezaji mbovu kuonekana wa thamani. Yeye ni
mchezaji mkubwa, vipi awe na wakala? Timu kubwa ni lazima zimtafute yeye, kwa
kuwa ubora wake hauhitaji mtu wa kumpigia kelele. Zlatan huyo!!
Chistiano
Ronaldo, pamoja na madoido yake yote, lakini hajawahi kuifikia Jeuri ya
Ibrahimovic. Balotelli, pamoja na utukutu wake wote, lakini hajawahi kumsogelea
Ibrahimovic. Nani anaweza kuwa rafiki yake? Kwa lipi? Kwanini? Labda Mourinho!
Wanaishi katika fikra moja. Pengine ni rahisi kuelewana.
Wakati
Lionel Messi akiwa hajui ni lini anaweza akamsamehe Ibrahimovic, kuna Zlatan
Ibrahimovic mwingine, tofauti kabisa na Ibrahimovic anayeishi katika kichwa cha
Pep Guardiola. Yule Ibrahimovic mwenye jeuri, dharau, kiburi na kila aina ya
majivuno. Zlatan huyu mwingine anashangaza kidogo, siyo Yule Ibrahimovic
tunayemjua.
Hajrudin Kamenja,
ana umri wa miaka nane. Anatokea katika taifa la Bosnia, katika kitongoji cha Vares,
kilomita kadhaa kulifikia jiji pendwa la Sarajevo. Dogo Hajrudin ametushangaza
kidogo. Kwa miaka sita sasa, amelazwa tu kitandani. Anasumbuliwa na kansa ya
mapafu ‘leukemia’. Na kwa mujibu wa ripoti ya madaktari, wanadai kuwa amebakiza
mwezi mmoja tu, kabla ya kufikwa na mauti.
Inasikitisha
sana, inaumiza pia. Mama yake Hajrudin ndiye anaumia kuliko wote. Amemwambia
mwanae, ni kitu gani cha mwisho angependa amfanyiwe kabla ya kufikwa na mauti? Simanzi
inaishia hapa sasa! Dogo Hajrudin amechagua kumuona Zlatan Ibrahimovic, ndiyo
kitu cha mwisho anachokipenda katika dunia hii. Hapahitaji mshangao hapa?
Kwanini
amekuwa Zlatan? Kwanini hakuwa Justin Beiber? Kwanini hakuwa hata Jaden Smith?
Labda Hajrudin anapenda sana mpira, sasa kwanini hakuwa Lionel Messi? Au
Christiano Ronaldo? Kwanini sio David Beckham pia? Kwanini Dogo amemchagua
Zlatan? Anapenda nini kwa Zlatan Ibrahimovic?
Unahitaji
kutulia kidogo, ili uweze kupata majibu yaliyotulia pia. Huenda Dogo Hajrudin
naye ameamua kuishi kama ndege, ameimba, tena ameimba kwa sauti, sauti ambayo
huenda itamkera sana Pep Guardiola. Ndiyo ukweli wake. Kwanini awe mnafiki?
Yule Zlatan jeuri, mwenye dharau na kiburi, ndiye kipenzi chake.
Najua sasa, Zlatan Ibrahimovic, atakuwa akipoteza muda
wake mwingi katika lile jumba lake la kifahari kule Jijini Paris, akili itakuwa
ikiwaza mambo mawili tu. Nini afanye kwa Dogo Hajrudin? Na lipi afanye, ili
watu waamini kuwa Yeye ni Tofauti na Ibrahimovic tuliyekuwa tukimfahamu? Mimi
nasubiri, tena nasubiri kwa hamu, hamu ya kutaka kujua ni nini ‘Ibra Cadabra’ atafanya.
No comments:
Post a Comment