Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Thursday, September 5, 2013

FELLAINI PEKEE NDIO KATUA UNITED KATI YA 13, MOYES KUNANI?



Katika 13, Fellaini pekee ndio katua United, Moyes kunani?
HARAKATI za Manchester United kuimarisha kiungo wakati wa kiangazi ziliendelea mpaka dakika ya mwisho ya dirisha la usajili.
Ushamba na kutokujua mambo kwa Mtendaji Mkuu Ed Woodward kulidhihirika wazi, kutokana na siku za mwisho za dirisha la usajili kutawaliwa na ofa za kuchanganyikiwa, majadiliano ambayo hayakuzaa matunda na taarifa za matapeli, huku kukiwa na dalili za kiangazi kupita bila usajili.
Hatimaye United walifanikiwa kumsajili Marouane Felleini kwa bei ya kupigwa ya pauni milioni 27.5 katika dakika za mwisho kabisa za usajili, lakini nini kilikuwa tatizo kwa Woodward na David Moyes mpaka hali kufika ilipofikia?
Bingwa linaangalia msako wa United kutafuta kiungo kuanzia kwa Cesc Fabregas mpaka usajili wa dakika za mwisho wa Ander Herrera na Sami Khedira. Na kujiuliza kama Mesut Ozil alikuwa sokoni kwa wiki mbili zilizopita kwa nini walimuacha aende Emirates?
CESC FABREGAS (Barcelona)
Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal ndiye alikuwa chaguo la kwanza la David Moyes pamoja na Fellaini – wakati kocha mpya akijaribu kuimarisha kiungo cha timu yake na kuongeza ufundi.
Inasemekana ilikuwa ndoto ya Moyes kutengeneza kombinesheni ya Michael Carrick, Cesc Fabregas na Fellaini kwenye kiungo cha timu hiyo.
United waliweka wazi nia yao ya kumtaka Fabregas, Moyes na Woodward walikuwa wakizungumza mbele ya vyombo vya habari kwamba wanafedha za kutosha na wanamtaka Fabregas wengi walitarajia kiungo huyo atakubali kutua Old Trafford kama ofa itatolewa, lakini Mhispaniola huyo hakuwa na mpango wa kuondoka Camp Nou.
Mabingwa wa England waliweka mezani ofa mbili, ofa ya pili ilikuwa zaidi ya pauni milioni 30, lakini Barcelona hawakutaka kumuuza. United walipoteza muda mwingi sana kutolea macho Fabregas na kusahau wachezaji wengine.
THIAGO ALCANTARA (Barcelona)
Bado haijawa wazi iwapo United walimtolea macho Thiago Alcantara (22) kwa nia ya dhati. Baada ya staa huyo kutua Bayern Munich, baba na wakala wa Thiago, Mazinho alitoboa siri kwamba Man United walikaribia kumsajili, lakini Thiago mwenye amekuwa akikanusha kufutwa na United.
Hatahivyo kipa wa United, David De Gea amewahi kukiri kwamba aliwahi kumshawishi Thiago kutua Old Trafford wakati wa fainali za Ulaya kwa ajili ya vijana chini ya miaka 22, nchini Israel wakati wa kiangazi.
Kinachojulikana hata hivyo ni kwamba Thiago alikuwa akitaka kuungana na kocha wake wa zamani Pep Guardiola katika klabu ya Bayern Munich. Akili ya United ilikuwa kwa Fabregas sana, lakini hata kama Moyes angeamua kumtolea macho Thiago, bado kinda huyo angetua Bayern.
LUKA MODRIC (Real Madrid)
United hawakufanya jitihada za dhati kumsajili Mcroatia huyu, lakini kiungo huyu wa zamani wa Spurs amekuwa kwenye rada za Man United tangu Real Madrid waliposhinda mechi ya Old Trafford katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ilikuwa wazi kabisa kwamba Modric alikuwa radhi kutua Old Trafford na kiungo huyo anakila kitu ambacho kinahitajika kwenye kiungo cha Man United.
Kama usajili wa Gareth Bale kwenda Madrid ungekamilika mapema, United wangeweza kufanikiwa kumnasa. Hatahivyo ndoto za Moyes kumnasa Modric zalizimika mara baada ya Xabi Alonso kupata majeruhi yanayomuweka nje kwa miezi mitatu. Hivyo umuhimu wake uliongezeka kwa Carlo Ancelotti.
ANDER HERRERA (Athletic Bilbao)
Mapema kabisa Athletic Bilbao waliweka wazi kwamba hawana mpango wa kufanya mazungumzo yoyote juu ya uuzwaji wa mchezaji, na kama United walikuwa wanamuhitaji basi walitakiwa kufikia dau la pauni milioni 30.5 lililoko kwenye mkataba wake.
Ni mara chache sana kwa Bilbao kuuza mchezaji wake chini ya bei yake iliyopo kwenye mkataba, Bayern Munich walimnasa Javi Martinez mwaka jana, lakini miamba hiyo ya Ujerumani iliwahi kukiri kwamba usajili huo ulikuwa mgumu zaidi kwenye historia ya klabu yao.
United kwa ujinga wao wakajaribu kupiga ‘sound’. Woodward na wafuasi wake inaonekana hawakusoma alama za nyakati. Taarifa zilizotoka Jumanne baada ya usajili kufungwa zinasema kwamba United walishindwa kutokana na sera ngu ya kodi, lakini klabu hiyo ilitakiwa kuifanyia utafiti Bilbao kabla ya kwenda kumtaka mchezaji wao.
Man United inasemakana walishafikia makubaliano binafsi na Herrera – ambaye alikuwa amekubali mkataba wa miaka mitano na kuingiza pauni milioni 3 mwaka, shughuli ilibaki wa Woodward kufikia dau la kwenye mkataba wake, lakini jaama akaona ni ghali sana.
Aibu zaidi ilikuja baada ya taarifa kuibuka kwamba matapeli watatu walitua kwenye ofisi za Chama cha Soka cha Hispania (LFP) na kudai ni wawakilishi wa Man United.
DANIELE DE ROSSI (AS Roma)
Baada ya mambo kuonekana yanazidi kwenda mrama, United wakapeleka ofa ya pauni milioni 10, Roma kwa ajili ya kiungo huyo Alhamisi iliyopita, lakini walitoswa na miamba hiyo ya Italia.
Kwa mara nyingine kushindwa kufanya utafiti kwa United kulionekana hapa - De Rossi alikuwa na wakati mgumu sana chini ya Zdenek Zeman, lakini sasa hivi chini ya Rudi Garcia mambo yanaonekana kukaa poa na hana mpango wa kuondoka kwenye klabu hiyo.
Kwa mara nyingine hapa tena walichemka na Woodward hakudiriki hata kurudi na ofa ya pili.
SAMI KHEDIRA (Real Madrid)
Masaa matano yakiwa yamebaki kabla ya dirisha kufungwa, taarifa zikaibuka kwamba United wamepeleka ofa ya euro milioni 40 kwa ajili ya Sami Khedira wa Real Madrid.
Hadi kufikia wakati huo, Ed Woodward alikuwa akitapatapa. Khedira ananguvu, stamina, lakini nia ya kutaka kumsajili jamaa huyu ilionekana ya ajabu hasa kutokana na Marouane Fellaini kwa njiani kutua Old Trafford. Kiungo cha Carrick, Fellaini na Khedira ingekuwa majanga na Mjerumani huyo hakuwa chaguo sahihi la kuziba nafasi ya Ander Herrera.
WESLEY SNEIJDER (Galatasaray)
Udhalilishwaji wa Moyes na Woodward katika usajili ulithibitika rasmi Jamanne, baada ya Galatasaray kudai kwamba Man United ‘wali-beep’ kwa Wesley Sneijder (29).
Galatasaray waliweka wazi kwamba Sneijder alipokea ofa ya United wiki mbili zilizopita, lakini wakaikataa kwa sababu hawakuwa na mpango wa kumuuza.
United waliwahi kukaribia kumsajili Mholanzi huyo mwaka 2011 kutoka Inter Milan, lakini mshahara wa pauni 200,000 kwa wiki alioutaka ulikuwa kikwazo.
Kwa nini United walimkataa United Ozil?
Man United waliwahi kupewa ofa ya kumsajili Ozil na Real Madrid wakati wa kiangazi, lakini wakamkataa, ila staa huyo mpya wa Arsenal alikuwa mchezaji sahihi kwa United, na kama United wangeamua kumchukua Mjerumani huyo angeenda Old Trafford badala ya Emirates.
Kuna hawa pia
Moyes alikuwa akihaha kutaka kumsajili Leighton Baines kutoka Everton na alianzia kutoa ofa ya pauni milioni 9 na kukwamia pauni milioni 15, Gareth Bale aliwahi kuhusishwa na United, lakini Real Madrid walikuwa na nafasi zaidi ya kumsajili, Kuna Fabio Coentrao pia, huyo alikuwa moja ya watu wa mwisho kufuatwa na United, usajili wake ulishindikana kutokana na kuchelewa kumalizika kwa taratibu.
Ezequiel Garay beki wa kati wa Benfica naye alikuwahi kutakiwa na United, dili lake lilianzishwa na Sir Alex Ferguson. Lakini Moyes hakuwa akimuhitaji na jamaa kabaki Lisbon. Cristiano Ronaldo hii ni ndoto ya mashabiki wa United, lakini Real Madrid hawana mpango wa kumuuza.
@@@
Je, Ozil alikuwa anahitajika Arsenal?
NA SELEMAN SHINENI
DUH! Ama kweli hakuna marefu yasiyo na ncha, kweli Arsene Wenger ambaye ubahili kwake ni kipaji ameacha na kutoa pauni milioni milioni 42.5 (sh bilioni 104.656) kumsajili mchezaji mmoja.
Rekodi ya usajili Arsenal ilikuwa ni pauni milioni 16.5 (sh bilioni 40.631) na ilikuwa ikishikiliwa na Santiago Cazorla ambaye Arsenal walimsajili msimu uliopita kutoka Malaga.
Safari hii Wenger amelipa zaidi ya mara mbili ya dau la Cazorla, kweli ile barua ya kundi la Black Scarf Movement ilimshitua Babu Wenger na kuona kibarua chake kitaota nyasi kama hatafanya usajili wa bei mbaya.
Sawa Ozil ni bonge la ‘mido’ amejaliwa kipaji cha hali ya juu, muongo muongo na anavitu adimu na ndio maana msimu uliopita pekee alipiga pasi za mwisho 30 akiwa Real Madrid.
Lakini swali linakuja Arsenal ilikuwa inahitaji kuvunja benki kwa Ozil? Ozil alikuwa akihitajika kiasi hicho pale Arsenal? Au ndiyo Wenger kafanya usajili wa kuwaridhisha Black Scarf Movement?
Najiuliza maswali haya kutokana na aina ya wachezaji ambayo Arsenal wanayo msimu huu, naamini kabisa hata kabla ya kutua kwa Ozil Arsenal ilikuwa imekamilika zaidi kwenye idara ya kiungo wa ushambuliaji.
Cazorla, Jack Wilshere, Tomas Rosicky na Alex Oxlade-Chamberlain wote wanaweza kucheza kama viungo washambuliaji, sasa unawaza Ozil naye wanini? Wakati kuna maeneo mengine kwenye timu hayajatimia.
Arsenal wanatatizo kubwa sana la kiungo mkabaji na ndio maana hata Mathieu Flamini kurudishwa bure kwenye timu na makinda kama kina Serge Gnabry na Gedion Zelalem wanakaa kwenye benchi la timu hiyo kama mchezaji aliyeuwanjani ataumia.
Mbali na Mikel Arteta na Aaron Ramsey eneo la kiungo wa ukabaji halina mchezaji wa ziada mwenye kiwango cha dunia, sasa kwa nini Wenger asingetafuta mtu wa kuongeza hapa, badala ya kusaini mchezaji mwingine mwenye akili ya kushambulia zaidi ya kulinda.
Ukiachana na kiungo wa ukabaji, Arsenal pia inatatizo kwenye beki yake ya kati, ambako ina Laurent Koscielny, Per Mertesacker na majeruhi Thomas Vermaelen, sasa kwa nini Wenger hakuongeza beki wa kati mwingine kusaidia na na hawa.
Straika pia ni tatizo kwa Arsenal, Olivier Giroud ndiyo ndiyo tegemezi wao pale, eti amembakiza Nicklas Bendtner kusaidiana naye pamoja na Yaya Sanogo.
Siyo kwamba Arsenal walikuwa hawatengenezi nafasi tatizo kwao lilikuwa ni mtu wa kumalizia, sasa hata baada ya ujio wa Ozil timu hiyo itaendelea kutengeneza nafasi, lakini mtu wa kufunga kwao bado itakuwa tatizo.
Arsenal ilikuwa ikihitaji Straika kama Michu, Christian Benteke, Demba Ba ambaye ukimtengenezea nafasi humuachi, lakini badala yake wameendelea kumng’ang’ania Giroud na kumuongezea mtu wa kumtengenezea nafasi.
Kati ya Cazorla, Wilshere, Rosicky na Ozil nani atapewa jukumu la kuchezesha timu au ndiyo wengine watasogezwa kucheza pembeni kama hilo likitokea nini kitawakuta kina Theo Walcott na Lukas Podolski?
Nikiiangalia Arsenal ilivyo, usajili wa Ozil ulitakiwa kuwa wa mwisho kabisa baada ya timu hiyo kuimarisha kiungo cha ukabaji, beki na safu ya ushambuliaji, lakini Wenger amenishangaza kwa kumwaga fedha nyingi kuimarisha sehemu imara kwenye timu yake.
Kitu pekee kilichonifurahisha kwenye usajili huu ni kitendo cha Wenger kutambua kwamba mpira wa sasa fedha ndiyo kila kitu, lakini siamini kama amemaliza ubahili wake kwa mchezaji sahihi.

No comments:

Post a Comment