VITA YA KIUCHUMI: TRA YAZIAMURU BANDARI KAVU KUFANYA KAZI SAA 24 KULINDA MAPATO



KATIKA kile kinachoonekana ni muendelezo wa mapambano ya kuimarisha uchumi wa Taifa, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, amewatupa uwanja wa mapambano wamiliki wa Bandari Kavu nchini (ICD) kwa kuwaamuru kuanza kufanya kazi saa 24 ili kuendana na kasi ya utoaji huduma za Forodha na ushindani wa kibiashara.

Akizungumza Februari 19, 2026, katika kikao kizito jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu Mwenda ameweka wazi kuwa Serikali haiko tayari kuona msongamano wa mizigo na ucheleweshaji wa biashara ukikwaza ukuaji wa uchumi. 

Amesema hatua ya kufanya kazi usiku na mchana ni mkakati wa makusudi wa kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi, huku akiahidi kuwa TRA tayari imejipanga na watumishi wa kutosha wa Forodha kuwezesha mapinduzi hayo.

“Niwatake kuhakikisha mnaongeza ufanisi katika ufanyaji wenu wa kazi kwa kujipanga kutoa huduma kwa saa 24. Sisi kama TRA tutatoa wafanyakazi wetu nanyi kwa upande wenu mjipange kwa vifaa na mengineyo; lengo ni kuongeza ufanisi wa nchi katika sekta hii muhimu,” amesisitiza Mwenda akionyesha msisitizo wa vita hiyo ya tija.

Kamishna Mkuu pia amevurumisha onyo kali dhidi ya "maadui wa ndani" wa uchumi, akiwatuhumu baadhi ya wamiliki wa ICD kwa kujihusisha na vitendo vya ukwepaji kodi. Amesema TRA inazo taarifa za kutosha kuhusu michezo hiyo michafu na kusisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhujumu mapato ya Serikali.

“Natambua kuna ukwepaji kodi katika ICD, hii haiwezi kukubalika. ICD zote zinatakiwa kuzingatia sheria; ni lazima tushirikiane kuzifanya ICD zionekane kuwa ni salama na hatutosita kuchukua hatua kwa wale watakaobainika,” amesema Kamishna Mkuu kwa sauti ya mamlaka.

Akichangia katika kikao hicho, Rais wa Sekta Binafsi (TPSF), Bi. Angelina Ngalula, amesema waendeshaji wa bandari kavu ni askari muhimu katika safari ya kuelekea Dira ya Taifa ya 2050, huku Mwenyekiti wa Wamiliki wa Bandari Kavu, Bw. Meleckzedeki Kichange, akisifu matumizi ya mifumo ya kidigitali kama TANCIS kama silaha muhimu iliyoongeza ufanisi na uwazi katika utendaji wao.

No comments