MKUU WA WILAYA YA ILALA AMALIZA MGOGORO WA MUDA MREFU WA ENEO LA MAKABURI PUGU
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amemaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi katika Mtaa wa Kinyamwezi Kata ya Pugu jijini Dar es Salaam ulihusisha uvamizi wa eneo la makaburi na ujenzi wa makazi ya watu kinyume na taratibu za mipango miji.
Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 13 mwaka 2026 mkuu huyo wa wilaya aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuhuruma Mabelya kwa lengo la kutoa ufumbuzi wa kudumu wa kero hiyo iliyokuwa imezua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo la Kimani.
Katika maelezo yake Mpogolo amebainisha kuwa eneo hilo lenye ramani ya upimaji namba E' 351 ya mwaka 2000 lilitengwa rasmi na Serikali kwa ajili ya matumizi ya makaburi tangu awali.
Amesema kuwa mgogoro huo ulichochewa na Bi. Elizabeth Mwakapangala ambaye alikuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu Saidi Shomari Loko baada ya kufungua kesi ya ardhi dhidi ya Halmashauri ya Jiji na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege akidai kumiliki eneo hilo.
Hata hivyo mkuu wa wilaya amefafanua kuwa hukumu iliyotolewa na Jaji Msafiri ilielekeza mlalamikaji kulipwa fidia na siyo kuuza eneo la makaburi wala kufukua mabaki ya miili ya watu na kuitupa kwenye maeneo yasiyo rasmi kama ilivyodaiwa na wananchi.
Aidha Mpogolo amesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria ya mipango miji mahakama haina mamlaka ya kufuta ramani za Serikali wala kuhoji mamlaka ya Rais ya kutwaa ardhi kwa manufaa ya umma.
Amesema hatua ya mlalamikaji kuuza viwanja katika eneo hilo na kuhamisha makaburi bila kufuata taratibu za kisheria na misingi ya kidini ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na miiko ya jamii.
Kutokana na hali hiyo Serikali imechukua hatua ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa awali wa mahakama huku ikiahidi kumchukulia hatua kali za kisheria mhusika kwa tuhuma za kufukua makaburi na kutupa mabaki ya miili ya marehemu.
Kwa upande wao wananchi wa eneo hilo wameeleza kuwa walielekezwa kutumia eneo hilo kwa ajili ya maziko tangu walipohamishwa kutoka Kipawa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Wakati huohuo mlalamikaji Bi. Elizabeth Mwakapangala amekanusha madai ya kufukua makaburi na kusisitiza kuwa eneo hilo ni mali yake halali kwa mujibu wa nyaraka anazomiliki kufuatia ushindi wa kesi yake ya mwaka 2022.
Pamoja na hayo mkuu wa wilaya amewahakikishia wananchi kuwa waendelee na shughuli zao kwa amani huku Serikali ikisimamia utekelezaji wa matumizi halali ya ardhi hiyo kama yalivyopangwa.
Post a Comment