Gamondi Akabidhiwa Rasmi 'Taifa Stars' Miaka Miwili
Zama mpya zimeanza rasmi ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' baada ya kocha Miguel Gamondi kusaini mkataba wa miaka miwili kuinoa timu hiyo. Hafla hiyo ya kihistoria imefanyika leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Gamondi, ambaye hapo awali alikuwa akikinoa kikosi hicho kama Kaimu Kocha Mkuu kufuatia kuondoka kwa Hemed Suleiman 'Morocco', sasa anapewa rungu kamili mbele ya mashuhuda wazito wa serikali na michezo.
Hafla hiyo imepambwa na uwepo wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerson Msigwa.
Historia AFCON 2025 Yaandika Mkataba
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Makonda amebainisha kuwa uamuzi wa kumpa Gamondi mkataba wa kudumu umetokana na rekodi yake ya kishindo aliyoiweka hivi karibuni nchini Morocco. Akiwa kocha wa muda, Gamondi aliiongoza Taifa Stars kufika hatua ya 16 bora ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), hatua ambayo Tanzania haikuwahi kuifikia katika historia yake.
"Serikali imeamua kumwajiri rasmi ili aiongoze timu yetu katika jitihada za kunyakua ubingwa wa AFCON 2027, ambapo Tanzania tutakuwa wenyeji kwa kushirikiana na wenzetu wa Afrika Mashariki," alisema Mhe. Makonda.
Ahadi ya Gamondi na Ushirikiano
Kwa upande wake, Miguel Gamondi amekiri kuwa kibarua hicho ni kikubwa lakini kinawezekana kwa ushirikiano wa wadau wote wa soka nchini.
"Hii ni dhamana kubwa, lakini niko tayari kuifanya. Kwa umoja na ushirikiano madhubuti kutoka kwa wadau wote, nina imani tutapata matokeo yatakayowafanya Watanzania wajivunie," alisema Gamondi kwa kujiamini.
Aidha, kocha huyo raia wa Argentina amemwagia sifa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji endelevu katika michezo na kuishukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa azma yao ya kuleta mageuzi kwenye soka.
Serikali Kubeba Mshahara
Kama ilivyokuwa utaratibu uliowahi kufanywa kwa makocha wa zamani wa Stars kuanzia enzi za Marcio Maximo, Serikali ndiyo itakayokuwa inawajibika kulipa mshahara wa Gamondi. Hatua hii inalenga kuiongezea nguvu TFF katika kusimamia masuala mengine ya kiufundi na kambi za timu hiyo.
Kibarua kikubwa cha Gamondi sasa ni kuanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya mashindano yanayokuja, huku macho ya Watanzania yakiwa yameelekezwa katika AFCON ya nyumbani mwaka 2027.
Post a Comment