RAIS DKT. SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA NAIBU KATIBU MKUU WA UN JIJINI ADDIS ABABA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina Mohammed jijini Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hiyo na umoja huo duniani.
Katika mazungumzo hayo Rais Samia ameeleza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kiutawala pamoja na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu hususan katika sekta za afya elimu maji safi usafi wa mazingira na juhudi za kupunguza umaskini kwa wananchi.
Aidha Rais Samia amethamini mchango unaotolewa na taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi za maendeleo nchini Tanzania kupitia ushirikiano wa kidiplomasia na misaada ya kisekta. Vilevile Rais ameeleza utayari wa Serikali kumpokea mjumbe maalum kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ambaye anatarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum wa kiongozi huyo wa juu wa umoja huo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Bi. Amina Mohammed amewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu Guterres na kubainisha kuwa Umoja wa Mataifa unathamini uhusiano wa karibu uliopo kati yake na Tanzania. Ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa mfano wa amani na utulivu barani Afrika huku akitambua jitihada za Rais Samia katika kuimarisha mifumo ya taasisi na kutatua changamoto mbalimbali kwa kutumia njia ya mazungumzo na maridhiano ya kisiasa.
Viongozi hao pia wametumia fursa hiyo kujadili umuhimu wa kufanya mageuzi ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa ili uendane na mazingira ya sasa pamoja na haja ya kuimarisha uratibu kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo yamehitimishwa kwa kugusia umuhimu wa ushiriki wa vijana katika masuala ya maendeleo ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Post a Comment