Van Persie (kulia) akivua jezi yake kumpa Santos |
LONDON, England
JEZI ya huyu jamaa ilimponza Andre Santos, akaonekana
ananuka ndani ya Emirates kuanzia kwa mashabiki hadi kwa kocha wake.
Hapa ni wakati Mbrazil huyo, alichukua jezi ya fowadi wa
zamani wa timu hiyo, Robin van Persie wakati wa mapumziko katika mchezo
uliofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester mwaka jana na
Arsenal kukumbana na kipigo cha mabao 2-1.
Kilichowauma zaidi mashabiki wa Arsenal ni kwamba, Van
Persie aliwafunga bao la mapema kabisa katika mchezo huo, ambapo hadi
mapumziko, tayari Washika Bunduki hao walikuwa nyuma kwa bao 1-0, hivyo kitendo
cha Santos kuchukua jezi ya RVP wakati walipokuwa wakitoka uwanjani kwenda
vyumbani, ilionekana kama usaliti.
Santos alihukumiwa kwa jambo hilo na kuonekana hafai tena,
licha ya kwamba kwenye mechi hiyo hakucheza kwa kiwango chake kilichobora,
lakini Wenger alimtupa nje kwenye kipindi cha pili na tangu hapo hakucheza tena
na kuamua kumtoa kwa mkopo kwa kumpeleka Gremio.
Baada ya kuona mwenzake ameponzwa kwa kitendo cha kuchukua
jezi ya Van Persie hadharani, mbele ya mashabiki wa timu hiyo pale la Old
Trafford, Theo Walcott sasa ametumia ujanja wa kuwaficha mashabiki pamoja na
kocha wake, ili kuichukua jezi ya swahiba wake huyo wa zamani, RVP.
Jumapili iliyopita, wakati Van Persie aliporejea Emirates
akiwa na kikosi chake kipya, mabingwa wa England, Man United, Theo Walcott
alimsubiri Mdachi huyo kwenye korido kumwomba jezi yake baada ya kuona kwamba
ingekuwa zengwe kubwa kama angebadilishana naye mbele ya macho ya mashabiki.
Na wakati alipokuwa akifanyiwa mahojiano baada ya mechi
hiyo, ambapo Theo Walcott alifunga bao la kuongoza kabla ya Van Persie
kusawazisha na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, winga huyo wa
England alionekana akiwa ametinga jezi ya Man United, iliyodhaniwa kuwa ni ya
fowadi huyo wa Uholanzi.
Ni kweli, jezi hiyo ilikuwa ni ya Van Persie, ambapo wawili
hao walibadilisha wakati wanapita kwenye korido la uwanjani hapo, Emirates
lakini safari hii ikiwa ni baada ya filimbi ya mwisho na si kama ilivyokuwa kwa
Santos, ambapo ilikuwa wakati wa mapumziko.
Santos aliwachefua mashabiki wa Arsenal kwasababu tu
alimfuata Van Persie na kumwomba jezi. Walcott yeye alisubiri pasipokuwa na
watu na kuchukua jezi ya Van Persie, ili mambo yasimgeuke na kuonekana kituko.
No comments:
Post a Comment