YANGA imemtema Kocha wa
makipa, Mfaume Athumani na kumrejesha Mkenya Razak Siwa, baada ya kumaliza
mkataba wa kuifundisha timu hiyo.
Siwa aliyewahi kuwa kocha
msaidizi wa timu hiyo, anatarajia kusaini mkataba mpya baada ya Yanga kurejea
kutoka Uturuki.
Akizungumza leo,
Mfaume alisema kuwa hataambana na kikosi cha timu hiyo kutokana na kumaliza
mkataba wake na klabu hiyo ambayo alishawahi kuitumikia katika miaka ya nyuma.
Alisema kuwa, mkataba wake na
Yanga umefikia ukingoni, hivyo ameamua kupumzika kwa muda katika masuala ya
soka.
“Nashukuru Wanayanga kwa ujumla wao kwa sababu
kwa muda wote ambao nimekuwepo hapa kama mchezaji, niliporejea kama kocha wa
makipa wamenipa ushirikiano wa hali ya juu,” alisema Mfaume.
“Kwa sababu hiyo sina sababu
ya kutofurahi kutokana na mafanikio ambayo niliyapata nikiwa na Yanga, naamini
ni mengi licha ya changamoto nyingi nilizokutana nazo kama kocha,” alisisitiza
Kocha huyo.
Alisema kuwa jambo ambalo anaweza
kujivunia ni kumfanya kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ kuwa namba moja kwenye
kikosi cha Yanga lakini zaidi ni kuunda nguvu kazi ya makipa bora Tanzania kwa
sasa.
“Nasema hivyo kwa sababu
ukiangalia Berko ambaye ameondoka, amekuwa ni moja ya tunda la kujivunia kwa
Wanayanga kwa muda mrefu, pia alikuwepo Shaban Kado pamoja na Said Mohamed
ambao wote naamini wanaweza kuwa makipa wa timu za taifa,” alisema Mfaume.
Hadi mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, Yanga imefungwa mabao 12 katika mechi 13
ilizocheza na kujikuta ikipata pointi 29, jambo lilionyesha kuwa Mfaume alifanya kazi
kubwa katika kuwanoa makipa hao.
No comments:
Post a Comment