TANZANIA YAPANDA NAFASI TATU FIFA



TANZANIA imepanda kwa nafasi tatu katika viwango vya ubora wa soka na kufika nafasi ya 112 duniani katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) vilivyotolewa Novemba 2026. 

Awali, ilikuwa ikishikilia nafasi ya 115 baada ya kushuka Oktoba mwaka huu. Kupanda kwake kunatokana na matokeo ya mechi za kalenda ya kimataifa ya Novemba 2026 katika kampeni ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. 

Taifa Stars ilipata suluhu dhidi ya vigogo Nigeria katika Uwanja wa Amaan, Unguja Novemba 17, mwaka huu na sare dhidi ya timu iliyopo ndani ya 30 bora duniani huongeza alama za FIFA. 

Kabla ya sare hiyo, Tanzania ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Nigeria ugenini Novemba 13 na Tanzania sasa ina takribani alama 1,170 ikilinganishwa na alama 1,166.82 ilizokuwa nazo kwenye orodha ya awali. 

Kenya ikiporomoka nafasi moja na kuwa ya 115 baada ya Jumanne kufungwa na Afrika Kusini kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027). 

Uganda nayo imeporomoka nafasi mbili hadi 89 lakini bado inaongoza kwa nchi za Afrika Mashariki ikiwa na alama 1,269.12, baada ya juzi kutoka sare na Botswana.

 Morocco imepanda nafasi mbili na kuongoza Afrika kwa viwango baada ya kupanda hadi nafasi ya tano dunia, na hivi karibuni iliifunga Niger mara mbili katika mechi za kufuzu kwa Afcon 2027. 

Simba wa Milima ya Atlasi imepanda kutoka nafasi ya awali ya saba na kuipita Ureno na mabingwa wa dunia mara tano, Brazil. Mabingwa wa dunia Hispania ndio wanaendelea kuongoza katika msimamo huo ikifuatiwa na Argentina, Ufaransa, England na Morocco. 

No comments