CAF yazindua nembo ya Afcon Pamoja 2027
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kushirikiana na wenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika, Tanzania, Kenya na Uganda limezindua rasmi nembo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Uzinduzi wa nembo hiyo ya Afcon Pamoja 2027 uliofanyika mtandaoni kwa wakati mmoja jana, unaashiria kuanza kwa sharashamra za kuelekea michuano hiyo mikubwa Afrika, zikiwa zimesalia siku 212 kabla ya kuanza Juni 19, 2027.
Nembo hiyo imebuniwa kwa taswira ya ‘Ngao’ ambayo ni alama inayopatikana katika nembo za taifa za nchi zote tatu ikiwakilisha utambulisho wa Afrika Mashariki, ulinzi, fahari na umoja, chini ya kaulimbiu: ‘Kuheshimu historia yetu, kusherehekea utamaduni wetu na kuashiria Afrika ya kesho’.
Umbo lake limeundwa kwa duara mbili zinazokatana, likipambwa kwa nakshi za shanga na Kombe la Afcon katikati lililozungukwa na ramani ya Afrika.
Nembo hiyo imebeba rangi za bendera za mataifa yote matatu ambazo ni nyekundu, nyeusi, kijani, njano na buluu. Aidha, CAF imezindua michoro 12 ya ziada inayotambulisha utamaduni wa kila nchi.
Nayo ni mistari ya mshazari kwa Tanzania, mistari ya mlalo kwa Kenya na Korongo mwenye taji kwa Uganda.
Jina ‘PAMOJA’ limetumika kuonesha mshikamano wa Afrika Mashariki kupitia Kiswahili katika kuandaa Afcon ya kihistoria kwa mara ya kwanza.

Post a Comment