Dar City Yaondoka Nchini Kuelekea Nairobi Kusaka Tiketi ya BAL 2027
Mabingwa wa mpira wa kikapu nchini Tanzania, Dar City Basketball Club, wameondoka leo tarehe 20 Novemba 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 3) jijini Dar es Salaam kuelekea Nairobi, Kenya.
Timu hiyo inakwenda kushiriki mashindano ya hatua ya Elite 16 (Road to BAL 2027 - Ukanda wa Mashariki) yanayotarajia kutimua vumbi kuanzia tarehe 23 hadi 29 Novemba 2026 katika ukumbi wa Kasarani Indoor Arena. Mashindano hayo ni jukwaa muhimu la kusaka timu zitakazofuzu kucheza Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu Barani Afrika (Basketball Africa League).
Wakiondoka nchini, wachezaji na viongozi wa Dar City waliagwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, aliyewapongeza kwa kujituma na kuwataka kupambana kwa moyo wote, nidhamu na uzalendo ili kuiwakilisha vyema nchi.
Mheshimiwa Mpogolo pia alieleza kufurahishwa kwake na mshikamano wa mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuisindikiza timu hiyo, akibainisha kuwa mapenzi hayo yanaonyesha thamani kubwa ambayo jamii inaipa Dar City katika kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini.
Katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda pia alikuwepo na kutoa neno kwa wachezaji.
Katika mashindano hayo ya Elite 16, Dar City imepangwa katika Kundi B ambapo itaanza kibarua chake tarehe 23 Novemba kwa kucheza dhidi ya Ferroviário da Beira ya Msumbiji. Baadaye tarehe 24 Novemba itashuka dimbani kumenyana na Namuwongo Blazers kutoka Uganda, kabla ya kuhitimisha mechi zake za hatua ya makundi tarehe 26 Novemba kwa kucheza dhidi ya Dolphins Basketball Club ya Botswana.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, Dar City imeweka historia kubwa katika mchezo wa mpira wa kikapu nchini baada ya kutwaa ubingwa wa Dar es Salaam (DBL) na kisha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Taifa (NBL) mara mbili mtawalia mwaka 2024 na 2025. Baada ya kushiriki hatua za kufuzu na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, timu hiyo inatafuta fursa nyingine ya kuendeleza wimbi lake la mafanikio na kuibeba tena bendera ya Tanzania katika ngazi ya Afrika.

Post a Comment