Rais Samia Aelekea Uturuki Kushiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31)



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo Jumanne, Novemba 10, 2026, kuelekea jijini Antalya, Uturuki, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31). 

Rais Samia ameagwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na viongozi mbalimbali wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kabla ya kuanza safari hiyo muhimu ya kikazi na kidiplomasia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, akiwa jijini Antalya, Rais Dkt. Samia atahutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (Antalya Leaders’ Summit). 


 






Kupitia jukwaa hilo la kimataifa, anatarajiwa kuwasilisha msimamo wa Tanzania pamoja na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Rais Samia atashiriki kikao cha ngazi ya juu kinachohusu matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika (High-Level Event on Clean Cooking in Africa). 

Ushiriki wake katika kikao hicho unalenga kuendeleza na kuimarisha ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo amekuwa kinara wake barani humo, ikilenga kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.

Mbali na shughuli za mkutano huo wa kimataifa, Rais Dkt. Samia atakutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip ErdoÄŸan. 

Mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia, kibiashara, na ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Uturuki.

Mkutano wa COP31 unaoendelea nchini Uturuki unawakutanisha viongozi wa dunia, wataalamu wa mazingira, na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama ili kujadili hatua za pamoja za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani kote.

No comments