WATAFITI WAKABIDHI RIPOTI YA MABAKI YA MKONGE KUZALISHA MBAO, MBOLEA NA NISHATI SAFI



Kiongozi wa Timu ya Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) cha jijini Arusha, Profesa Anthony Mshandete, ameeleza kuwa utafiti wa awamu ya pili waliofanya wa zao la mkonge umebaini kuwa maganda na mabaki ya mkonge yana uwezo mkubwa wa kubadilishwa kuwa bidhaa za kimkakati zenye faida kubwa kiuchumi.

Bidhaa hizo ni kama vile mbao, mbolea bora ya kilimo, pamoja na nishati mbadala ikisheheni joto na gesi. 

Utafiti huo uklifanywa na wataalamu kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Akikabidhi ripoti ya utafiti amesema pia kwamba mabaki hayo yanafaa kwa utengenezaji wa chakula cha mifugo, kukuza viwanda vya uzalishaji wa protini, na kutumika kama malighafi katika matumizi mengine mbalimbali ya viwandani. 

Utafiti huo ulioratibiwa na NM-AIST unatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa kiikolojia na kiuchumi kwa kufungua fursa mpya za kuongeza thamani katika sekta ya mkonge nchini.



Akiipokea ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saad Kambona, alisema kuwa kwa muda mrefu nchi imekuwa ikitumia asilimia nne pekee ya zao la mkonge wakati wa uchakataji huku asilimia 96 zilizobaki zikitupwa kama taka. 

Kambona alibainisha kuwa Bodi imeridhishwa na matokeo hayo ya awali yanayokwenda kuongeza matumizi ya mkonge, na kwamba hatua inayofuata ni kuandaa mkutano mkubwa utakaowashirikisha wadau wengi zaidi pamoja na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuhakikisha matokeo ya utafiti huo yanafanyiwa kazi kivitendo ili wakulima na wawekezaji waweze kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na mazao na mabaki ya mkonge kwa njia endelevu.

No comments