BAGAMOYO KUSHUHUDIA MLIPUKO WA SANAA: TaSUBa Yeleza Upekee wa Tamasha la 44


 


Mji wa kihistoria wa Bagamoyo unatarajiwa kuwaka moto wa sanaa na utamaduni kuanzia kesho kufuatia kuanza kwa Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo. Likiwa ni jukwaa kubwa linalokusanya wasanii, wadau, na vikundi kutoka ndani na nje ya nchi, tamasha la mwaka huu linakuja na sura mpya na fursa tele za kibiashara na kiutamaduni. Mwandishi wetu Beda Msimbe alipata fursa ya kuketi na kufanya mahojiano maalumu na Naibu Mkuu wa Chuo cha TaSUBa, Bw. Gabriel Kiiza, ambaye anafunguka kwa undani kuhusu historia, maboresho, na kile ambacho Watanzania na wageni wanapaswa kukitarajia. Hii ni sehemu ya mahojiano .

 

SWALI:

Mbali na kubadilishana uzoefu na ujuzi wa kisanifu, tamasha hili linatoa fursa gani za moja kwa moja za kiuchumi, masoko, na mitandao ya kibiashara kwa wasanii wanaoshiriki na wakazi wa mji wa kihistoria wa Bagamoyo?

JIBU:

Tamasha linatoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wasanii, wajasiriamali na wakazi wa Bagamoyo. Mbali na kubadilishana uzoefu na ujuzi wa kisanaa, Tamasha hili lina manufaa yafuatayo:

•        Fursa za masoko kwa wasanii: Tamasha linawapa wasanii nafasi ya kuonesha na kuuza kazi zao za sanaa, kama vile vinyago, michoro, uchongaji, mavazi ya asili na kazi nyingine za ubunifu. Pia, wanapata fursa ya kutangaza vipaji na bidhaa zao kwa hadhira kubwa kutoka ndani na nje ya nchi.

•        Fursa za mitandao ya kibiashara: Kupitia tamasha hili, wasanii wanakutana na wadau wa sanaa, wawekezaji, wazalishaji wa maudhui, waandaaji wa matukio na wanunuzi wa kazi za sanaa. Mahusiano haya yanaweza kufungua milango ya kupata mikataba, ushirikiano wa kibiashara na fursa za kazi hata baada ya Tamasha kumalizika.

•        Kuongeza kipato kwa wakazi wa Bagamoyo: Tamasha huongeza mahitaji ya huduma mbalimbali, zikiwemo malazi, chakula, usafiri, bidhaa za matumizi na huduma za utalii. Hali hii huwapa wafanyabiashara, wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni, mama lishe, madereva wa bodaboda na tax pamoja na watoa huduma wengine nafasi ya kuongeza wateja na mapato yao.

•        Kukuza utalii na biashara za kiutamaduni: Tamasha linaitangaza Bagamoyo kama kitovu cha historia, sanaa na utamaduni. Wageni wanapata fursa ya kutembelea maeneo ya kihistoria, kununua bidhaa za asili na kutumia huduma za utalii, jambo linaloweza kuchochea ukuaji wa biashara.

•        Fursa za ajira na kujiajiri: Maandalizi na utekelezaji wa tamasha huibua mahitaji ya huduma za kiufundi, upambaji, upigaji picha na video, matangazo, usimamizi wa matukio na biashara ndogondogo. Hivyo, vijana na wabunifu hupata kazi za muda au kujenga fursa za kujiajiri.

•        Kupanua soko la sanaa za Kitanzania kimataifa: Ushiriki wa wasanii kutoka nchi mbalimbali unawawezesha wasanii wa Kitanzania kutangaza kazi zao nje ya mipaka, kutambua mahitaji ya masoko ya kimataifa na kujifunza namna ya kuboresha bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko pana zaidi.

Kwa ujumla, Tamasha la Bagamoyo si jukwaa la burudani na ubadilishanaji wa utamaduni pekee, bali pia ni kichocheo cha uchumi wa sanaa na ubunifu. Linatoa nafasi ya kukuza biashara, kuongeza kipato, kutengeneza ajira na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya wasanii na jamii. Manufaa haya yanaweza kuendelea hata baada ya tamasha kumalizika iwapo mahusiano na fursa zinazopatikana zitaendelezwa.

 

SWALI:

Bagamoyo ina utajiri mkubwa wa kihistoria na kiutamaduni. Tamasha hili linatumikaje kukuza utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) na kuhifadhi turathi za taifa letu kwa kizazi cha sasa na kijacho?

JIBU:

Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lina mchango mkubwa katika kukuza utalii wa kiutamaduni na kuhifadhi turathi za taifa letu. Bagamoyo ni mji wenye historia tajiri inayohusiana na biashara ya watumwa, shughuli za wamisionari, usanifu wa majengo ya kihistoria pamoja na sanaa na utamaduni wa jamii ya watu wa Pwani.

Kupitia Tamasha hili, tunapata fursa ya kuutangaza utajiri wa kihistoria na kiutamaduni wa Bagamoyo kwa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali, ambao wanapata nafasi ya kujifunza historia yetu kupitia ngoma za asili, muziki, maigizo, filamu, maonesho ya sanaa na shughuli nyingine za kiutamaduni.

Aidha, tamasha linachochea utalii kwa kuwavutia wageni kutembelea maeneo ya kihistoria ya Bagamoyo, hivyo kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia huduma za malazi, chakula, usafiri, bidhaa za sanaa na kazi za mikono.

Katika suala la uhifadhi wa turathi, Tamasha linasaidia kurithisha maarifa, mila, desturi na sanaa za jadi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Vijana wanapata nafasi ya kujifunza na kuthamini utamaduni wao, huku wasanii na wabunifu wakipata jukwaa la kuendeleza na kuutangaza utambulisho wa Kitanzania.

SWALI:

Ni yapi hasa malengo makuu ya kimkakati ambayo TaSUBa imeyapanga kufikia kupitia tamasha hili la 44 kwa upande wa maendeleo ya sanaa na utamaduni wa Tanzania?

JIBU:

Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lina malengo ya kimkakati yanayolenga kuendeleza sanaa na utamaduni wa Tanzania, kukuza vipaji na kuimarisha ushirikiano kati ya wasanii wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa TaSUBa, malengo makuu tunayotarajia kuyafikia kupitia tamasha hili ni pamoja na, kwanza, kuibua na kukuza vipaji vya wasanii, hususan vijana. “Tunataka kutoa jukwaa kwa wasanii chipukizi na wenye uzoefu kuonesha uwezo wao, kujitangaza na kupata fursa za kukuza taaluma zao katika fani mbalimbali za sanaa”.

Pili, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa sanaa na utamaduni wa Tanzania. Kupitia maonesho ya ngoma za asili, muziki, maigizo, sanaa za ufundi na shughuli nyingine za kiutamaduni, tunalenga kuhakikisha utamaduni wetu unaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, huku ukikua sambamba na mabadiliko ya wakati.

Tatu, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sanaa na utamaduni. Tamasha linatoa fursa kwa wasanii wa Tanzania kukutana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya za ubunifu na kujenga mitandao itakayowawezesha kupanua wigo wa kazi zao.

Nne, tamasha ni fursa ya wasanii kutangaza na kuuza kazi zao, kuunganisha sanaa na biashara, pamoja na kufungua fursa za ajira na kujipatia kipato kupitia vipaji vyao.

Tano, tamasha lina lengo la kuitangaza Tanzania kupitia sanaa, utamaduni na utalii. Kwa kutumia nafasi ya Bagamoyo kuwa mji wenye historia muhimu ya urithi wa utamaduni, tunalenga kuvutia wageni na wadau kutoka ndani na nje ya nchi, huku tukitangaza vivutio vya kihistoria na kiutamaduni vilivyopo katika eneo hilo.

Tamasha hili ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya TaSUBa ya kutoa mafunzo, kukuza utafiti na kuendeleza taaluma za sanaa na utamaduni. Pia, linawapa wanafunzi fursa ya kuonesha kwa vitendo ujuzi walioupata kupitia mafunzo yao.

 

SWALI:

Je, uwepo wa nchi hizi za nje unaleta ladha gani mpya katika kubadilishana utamaduni kati ya Tanzania na mataifa hayo?

JIBU:

Uwepo wa nchi za nje katika Tamasha hili la Bagamoyo unaleta ladha mpya katika kubadilishana utamaduni kwa sababu unatoa fursa kwa Tanzania na mataifa hayo kuoneshana utajiri wa sanaa, mila na desturi zao. Kupitia ngoma za asili, muziki, maigizo, mavazi ya kitamaduni na aina mbalimbali za maonesho, tunapata nafasi ya kujifunza tamaduni tofauti na kuelewa namna watu wa mataifa mengine wanavyoishi na kujieleza kupitia sanaa.

Aidha, ushiriki huu unawawezesha wasanii wa Tanzania kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka nchi mbalimbali, kujifunza mbinu mpya za ubunifu na kuanzisha ushirikiano wa kisanaa unaoweza kufungua fursa za kimataifa.

SWALI:

Mbali na mastaa wakubwa, TaSUBa imeweka mfumo gani wa kuhakikisha wasanii chipukizi au vikundi vya mikoani vinapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao pembeni ya mastaa hao?

JIBU:

TaSUBa inatoa nafasi ya kipekee kwa wasanii chipukizi na vikundi kutoka mikoa mbalimbali nchini kupitia Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambayo ni fursa kwa vipaji vipya kuonesha uwezo wao, kujitangaza na kukutana na wadau mbalimbali wa sanaa.

Kupitia maonesho ya muziki, ngoma za asili, maigizo, sarakasi, filamu na sanaa nyingine, wasanii wanapata nafasi ya kuonyesha kazi zao mbele ya hadhira pana. Aidha, kukutana na wasanii wenye uzoefu kunawapa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kikazi.

Lengo la TaSUBa ni kuhakikisha jukwaa hili linakuwa daraja la kukuza vipaji, kuibua vipaji vipya na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Kitanzania. Hivyo, wasanii chipukizi na vikundi kutoka mikoani wanahimizwa kutumia fursa hii kuonesha ubunifu wao na kuchangia ukuaji wa tasnia ya sanaa nchini.

 

SWALI:

Kwa wananchi, wapenzi wa sanaa, na wadau mbalimbali watakaotembelea viwanja na kumbi za TaSUBa kuanzia tarehe 28 Oktoba 2026, ni mambo gani ya kipekee na maboresho mapya wanayopaswa kuyatarajia katika tamasha hili la 44 ambayo hayakuwepo huko nyuma?

JIBU:

Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linatarajiwa kuwa jukwaa la kipekee la kukutana kwa Tamaduni, kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufurahia burudani mbalimbali. Kuanzia tarehe 28 hadi 31 Oktoba 2026, wananchi na wadau watakaotembelea viwanja vya TaSUBa watarajie mlipuko mkubwa wa burudani ambao utapambwa kwa maonesho ya sanaa, muziki, ngoma za asili, maigizo, filamu na sarakasi kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, tamasha hili litatoa fursa kwa wageni kujifunza kuhusu tamaduni mbalimbali, vipaji vipya na ubunifu unaoendelea kukua katika tasnia ya sanaa.

Eneo la vyakula pia litawawezesha wageni kufurahia vyakula mbalimbali, ikiwemo samaki choma, nyama choma na vyakula vya asili.

Jambo la kipekee ni fursa ya wananchi kukutana moja kwa moja na wasanii, wataalamu na wadau wa sanaa, kujadiliana kuhusu fursa zilizopo katika tasnia na kubadilishana mawazo yatakayochochea maendeleo ya sanaa na utamaduni nchini.

Hivyo, tunatoa wito kwa wananchi wote, wapenzi wa sanaa, vijana, familia na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hili.

mwisho

 

 

 


No comments