TANZANIA YAWEKA HISTORIA WILDSCREEN: FILAMU YA CHAMELEON CORRIDORS YASHINDA TUZO
Tanzania imeweka alama tena kwenye ulingo wa kimataifa wa utengenezaji filamu baada ya filamu ya Chameleon Corridors, iliyoongozwa na mtengenezaji filamu wa Kitanzania Jigar Ganatra, kushinda Tuzo ya Filamu Fupi Bora zaidi ya Panda katika tuzo maarufu za Wildscreen Panda Awards 2026, zilizofanyika mjini Bath, Uingereza hivi karibuni.
Filamu hiyo inakuwa kazi ya kwanza kutoka Afrika kushinda katika kipengele hicho katika historia ya utoaji wa tuzo hizo.
Ikielezwa mara kwa mara kama Tuzo za Oscar za Kijani (Green Oscars) katika utengenezaji filamu za wanyamapori, Wildscreen Panda Awards ni miongoni mwa tuzo za heshima za juu za kimataifa katika sekta hiyo.
Shindano la mwaka huu lilivutia jumla ya kazi 624 kutoka nchi 46 katika vipengele 18 vya tuzo.
Ikiwa imeandaliwa na taasisi ya AFRISOS kwa ushirikiano na Schoolyard Films pamoja na Amberjack Films, Chameleon Corridors ilitengenezwa na timu ya utayarishaji ya Kitanzania pekee. Filamu hiyo ilipata uteuzi katika vipengele vinne, vikiwemo Filamu Fupi, Watoto, Athari (Impact), na Kipaji Chipukizi, kabla ya kujinyakua ushindi huo wa kihistoria.
Mafanikio haya ya Chameleon yanaendeleza rekodi ya kipekee kwa Tanzania katika Tuzo za Panda: Mwaka 2024, Erica Rugabandana alishinda Tuzo ya Kipaji Chipukizi kupitia filamu ya Living with Lions; mwaka 2025, Bazili Kessy alipokea Tuzo ya Utambuzi wa Umahiri wa Uwanjani na mwaka huu 2026, Chameleon Corridors ya Jigar Ganatra imeshinda Tuzo ya filamu fupi.
Miaka mitatu, washindi watatu kutoka Tanzania, ikionyesha utambuzi unaozidi kukua wa kimataifa kwa kipaji cha Tanzania katika utengenezaji filamu za wanyamapori.
"Hii ni zaidi ya tuzo kwa ajili ya filamu moja. Ni sherehe ya kile ambacho watengenezaji filamu wa Kitanzania wanaweza kukifikia pale tunapopata fursa ya kusimulia hadithi zetu wenyewe. Afrika ina vipaji vya ajabu, maarifa na mitazamo ambayo dunia inastahili kuiona. Tunatumai mafanikio haya yanafungua milango mingi zaidi kwa kizazi kijacho cha wanasimulizi wa hadithi wa Kiafrika." anasema Jigar Ganatra, Mkurugenzi wa Chameleon Corridors na Mwanzilishi wa AFRISOS
Ikiwa imetengenezwa katika milima ya tao la mashariki nchini Tanzania , filamu hiyo fupi ya dakika 20 inasimuliwa na kinyonga mwenye hekima na inachunguza uhusiano uliopo kati ya watu, wanyamapori na misitu wanayoitegemea.
Katika kiini cha hadithi hiyo yupo Anna, msichana mdogo ambaye dhamira yake ya kurejesha msitu unaotoweka inaakisi harakati kubwa za urejeshaji misitu zinazoongozwa na jamii zinazowashirikisha wakulima zaidi ya 300 katika Milima ya Nguru.
Ikiwa inachanganya utengenezaji filamu za historia ya asili na mitazamo ya kienyeji, maarifa ya jadi na usimulizi wa hadithi za ubunifu, filamu hiyo inatoa mtazamo wa Kitanzania wa kipekee katika filamu za makala za wanyamapori.
Bodi ya Filamu Tanzania kupitia instagramu yake imetoa pongezi za dhati kwa timu nzima iliyofanikisha ushindi huo, ikibainisha kuwa mafanikio haya ni kielelezo cha uwezo, ubunifu na ubora unaozidi kukua wa watengenezaji filamu wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Bodi imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau ili kujenga mazingira wezeshi yatakayowezesha vipaji na kazi za Watanzania kufikia masoko na majukwaa ya kimataifa.mwisho

Post a Comment